Kiswahili paper 2 Questions and Answers - Form 3 End Term 1 Exams 2023

Share via Whatsapp
  1. UFAHAMU (ALAMA 15)
    Soma makala yafuatayo kisha ujibu maswali.


    Hulka ya binadamu katika maisha yake ni matarajio ya kupata mambo mazuri zaidi kwa kadiri anavyozidi kuishi duniani. Hulka hiyo haiepukiki kwa mtu yeyote ilimradi yungali hai duniani.

    Wapo watu wanaofanya kazi kufa na kupona ili kubadili maisha yao au kujiletea hali, watu hawa matumaini yao ni kuona wanaishi vizuri zaidi kesho kuliko walivyoishi jana.

    Kadhalika wavivu nao ambao wana tabia ya kutopenda kujishughulisha kutafuta maisha, mawazo yao yanabaki palepale kutarajia maisha bora. Mtazamo huo wa matarajio ya maisha bora uko pia kwa vyombo vyenye dhamana kwa maisha ya watu katika jamii kama vile serikali. Tofauti na mtu binafsi, ambaye huota ndoto hizo peke yake, serikali hushirikisha mipango inayojiwekea ya kuleta hali bora katika jamii, inafanikiwa.

    Ndani ya serikali kuna wadau (washika dau) mbalimbali wenye majukumu ya kuhakikisha kuwa mipango inayowekwa inasimamiwa na kutekelezwa katika muda unaotakiwa, ili kukidhihaja ya kuleta maendeleo katika jamii, tofauti na mtu binafsi ambaye wakati mwingine husimama peke yake katika kutekeleza malengo yake hayo.

    Serikali ina nafasi nzuri ya kutekeleza malengo kwa kutumia rasilimali zake wakiwemo watu, madini, misitu, ardhi na nyingine nyingi. Matumizi haya ya rasilimali katika kuleta maendeleo, ni jambo muhimu sana katika kutekeleza mipango yake. Kuna sababu kadha zinazotufanya tuishi miaka nenda miaka rudi tukiwa na kiu ya maendeleo na ndoto ambazo zinashindwa kutimia.

    Tatizo kubwa lililopo ni kwamba pamoja na kuwa na wataalamu wazuri na sera nzuri, tumeshindwa kuzitekeleza, badala yake tumekuwa mabingwa zaidi wa kuelezea sababu za kushindwa kutekeleza sera hizo kuliko kujikosoa kwa uzembe unaotufanya na kusababisha kushindwa kutekelezwa kwa sera hizo. Jambo hilo limechangia kurudisha nyuma maendeleo ya nchi yetu kwa miaka mingi. Mipango mingi inayopangwa na serikali, mara nyingi imekwama, matokeo yake badala ya kutafuta udhaifu uliokwamiza kutekelezwa kwa mipango hiyo, nguvu zaidi zinaelekezwa kuhalalisha sababu za kushindwa. Tunapaswa kujiuliza ni kwa nini tumefikia hapo? Tukipata jibu tukae chini tusioneane aibu, tunyosheane vidole usoni. Tusioneane haya katika kuleta maendeleo.
    (Kutoka gazeti la Majira, Oktoba 31, 2003)

    Maswali
    1. Upe ufahamu huu anwani mwafaka. (alama 1)
    2. Binadamu wote wana hulka moja. Ifafanue. (alama 2)
    3. Eleza jinsi serikali ilivyo na uwezo wa kutekeleza ndoto zake (alama 3)
    4. Kulingana na taarifa, ni kwa nini serikali hushindwa kuzitekeleza sera zake(al 2)
    5. Mwandishi anatoa wito gani katika aya ya mwisho? (alama 2)
    6. Andika methali mbili zinazohusiana na aya mbili za mwisho. (alama 2)
    7. Eleza maana ya vifungu vifuatavyo kwa mujibu wa taarifa. (alama 3)
      1. Kukidhi haja
      2. Kiu ya maendeleo
      3. Tunyosheane vidole usoni
  2. MUHTASARI (Alama 15)
    Soma taarifa ifuatayo kisha ujibu maswali yanayofuata.
    UFUPISHO

    Katiba mpya imeipa lugha ya Kiswahili hadhi nyingine kuifanya kuwa lugha rasmi kando na kuwa ni lugha ya taifa. Mabadiliko haya muhimu yana changamoto kadhaa.

    Kwanza kabisa lugha ya Kiswahili sasa itashindania nafasi sawa na ile ya Kiingereza katika shughuli za kikazi. Swala hapa linahusu majukumu ambayo lugha hizi zitatekeleza. Je, lugha hizi zinatumika mtawalia katika shughuli za kikazi au zitatengewa majukumu maalum?

    Lugha ya Kiswahili itachukua nafasi ipi? Kiingereza kitaachiwa nani tukizingatia kuwa kwa muda mrefu lugha ya Kiingereza ndiyo imekuwa lugha tawala katika mazingira haya? Je, wananchi wataweza kufanya maombi kwa lugha ya Kiswahili kando na kuendesha mawasiliano ya kiofisi kwa lugha hii? Kwa kifupi ili kusitokee mgongano wa matumizi ya lugha hizi mbili ni muhimu sana kwa watunga - sera kueleza kinagaubaga mawanda ya matumizi ya lugha hizi mbili katika mazingira ya kikazi.

    Changamoto nyingine na muhimu ni kiwango cha maandalizi ya wananchi katika kuyapokea mabadiliko haya. Kwanza, wananchi wanafaa wafahamishwe kuhusu haki yao ya kutumia lugha hii katika mazingira ya kazi. Si ajabu kuwa wao hawana habari kuhusu mabadiliko haya ya kisera. Watumishi wa umma nao wanastahili kupewa mafunzo maalumu kuhusu mbinu za mawasiliano katika Kiswahili ili waendeshe shughuli zao vizuri.

    Kwa upande mwingine, vyuo vikuu pamoja na taasisi nyingine za mafunzo zinastahili kutoa kozi ya lazima katika lugha ya Kiswahili kwa wanafunzi wanaojiunga nazo ili kuwaandaa kwa mahitaji haya mapya ya kikatiba. Kadhalika, serikali inastahili kuwaandaa wataalamu zaidi wa lugha ya Kiswahili ambao watahusika katika kuwafunza wanaohusika na utekelezaji sera.

    Kuna haja pia ya wataalamu wa lugha kuandika vitabu zaidi kwa lugha ya Kiswahili ambavyo vitatoa mafunzo kuhusu mbinu mbalimbali za mawasiliano. Shughuli hii iambatane na ile ya kutafsiri vitabu vilivyoandikwa kwa lugha nyingine kwa ile ya Kiswahili.

    Kwa muda mrefu sasa, kumekuwa na tatizo la mitazamo hasi miongoni mwa wananchi kwa lugha ya Kiswahili. Baadhi ya wananchi wamekuwa na sababu zao za kutoitumia lugha hii wakishikilia kuwa lugha yenyewe ni ngumu.

    Aidha, wananchi wengine wamekuwa na uzoefu wa kuzungumza lugha ya kiingereza au lugha nyingine za kigeni huku wakitoa nafasi finyu kwa lugha ya Kiswahili. Serikali Inastahili kutafuta njia ya kuwahimiza wananchi wote kuionea fahari lugha ya Kiswahili, waipende na kuielewa vizuri.

    Ni muhimu kufanywe kila juhudi kuhakikisha kuwa wananchi wanatumia Kiswahili sanifu ili wasije wakakivuruga kwa kukiendeleza visivyo au kwa kukiharibu kwa kijilugha cha sheng au kwa lugha za kienyeji.

    Vile vile, ni muhimu wananchi watambue kuwa nchi yetu ya Kenya ndiyo kitovu cha lugha hii na hivyo basi wafanye kila juhudi kuitumia ipasavyo ili tusionekane kuwa watumwa katika lugha yetu asili. Tunahitaji viongozi vielelezo nchini ambao wanazungumza Kiswahili sanifu kwa madoido na ufasaha sio tu katika ulingo bali pia katika nyanja nyingine za maisha.

    Kwa hivyo viongozi wetu wajiepushe na matumizi ya Kiswahili chapwa ili wananchi wahimizike kuzungumza Kiswahili kwa ufasaha. Ingekuwa hata bora ikiwa wangepewa kipaumbele katika kupokea mafunzo kabambe katika lugha hii. Pengine tungejifunza mengi kutoka nchi jirani ya Tanzania ambayo kwa kiasi kikubwa ilifaulu kurasmisha Kiswahili na kuleta umoja wa kitaifa.

    MASWALI
    1. Fafanua changamoto zinazoikumba lugha ya Kiswahili kama lugha rasmi. (Maneno 70)
      (alama 6, 1 mtiririko)
      Matayarisho.
      Jibu
    2. Mwandishi ametoa mapendekezo kuhusu namna ya kuimarisha matumizi ya Kiswahili nchini. Yafafanue.
      (Maneno 80) (alama 7, 1 mtiririko)
      Matayarisho
      Jibu
  3. MATUMIZI YA LUGHA
    1. Taja sauti mbili za nazali. (Al 2)
    2. Taja aina mbili za mofimu na utolee mfano mmoja mmoja (al 2)
    3. Tunga sentensi yenye kitenzi kishikirishi kipungufu (al 2)
    4. Tunga sentensi moja ukitumia kihisishi na nomino maalum (al 2)
    5. Eleza maana ya chagizo na utunge sentensi moja kuonyesha maana yake (al2)
    6. Tumia “amba” rejeshi katika sentensi ifuatayo (al 2)
      Mchezaji ninayempenda ni Messi
    7. Yakinisha sentensi ifuatayo. (al 2)
      Asingepigiwa kura, asingekuwa rais wa Kenya.
    8. Unda nomino kutokana na vitenzi vifuatavyo (al 2)
      1. Tafakari
      2. Sujudu
    9. Badilisha sentensi ifuatayo iwe katika hali ya kuamuru katika wingi (al. 2)
      Njoo hapa.
    10. Andika katika msemo wa taarifa
      “Naapa ya kwamba nitatumikia wananchi wa Kenya na nitakuwa mwaminifu,” Rais mteule alisema (al 2)
    11. Onyesha vishazi katika sentensi ifuatayo (al2)
      Uchaguzi uliofanywa nchini Kenya ulikuwa wa amani
    12. Bainisha aina za shamirisho katika sentensi . Shule nzuri ilijengewa wanafunzi kwa matofali (al 3)
    13. Changanua sentensi ifuatayo ukitumia jedwali (al 4)
      Walimu shupavu walifunza vizuri lakini wanafunzi hawakupita mtihani
    14. Eleza sifa mbili za sentensi ambatano na utoe mfano mmoja (al 3)
    15. Eleza matumizi tofauti ya kiambishi ‘ni’ katika sentensi ifuatayo (al 2)
      Nitasoma kwa bidii shuleni
    16. Tunga sentensi moja ukitumia neno ‘gani’ kama (al 2)
      1. Kiwakilishi
      2. Kivumishi
    17. Tunga sentensi ukitumia kitenzi ‘la’ katika hali ya kutendesha (al 2)
  4. ISIMU JAMII (al 10)
    “Karibu wageni karibuni
    Come and learn with us lugha ya Kiswahili
    Nyote mtabenefit sana”
    “Kwa nini?”
    “Kwa sababu it’s a national language”

    Maswali  
    1. Lugha ngapi zimetumika katika muktadha hii? (al 2)
    2. Mtindo wa kutumia lugha zaidi ya moja katika mazungumzo huitwaje? (al 2)
    3. Mzungumzaji mwenye uwezo wa kutumia lugha zaidi moja anaitwaje? (al 2)
    4. Taja sababu za wazungumzaji kutumia lugha zaidi ya moja (al 4)

MARKING SCHEME

UFAHAMU

  1. Maendeleo / Jinsi ya kuleta maendeleo    (alama 1)
  2. Hulka ya kutarajia mambo mazuri zaidi  maishani.  (alama 2)
    wanafanya kazi kufa kupona na kuwa na matumaini ya kuishi vizuri zaidi kesho
  3. Jinsi serikali iliyo na uwezo wa kutekeleza ndoto zake
    1. Inafanya mipango ya kuleta hali bora kwa
    2. Kushirikisha wadau ambao wana majukumu ya kusimamia na kutekeleza mipango katika muda unaotakiwa.
    3. Inatumia rasilimali zake k.v. madini, misitu, ardhi   (alama  3×1 = 3)
  4.  
    1. Uvivu / Kutopenda kujishughulisha na kazi
    2. Kuelekezeana lawama / Kuegemea zaidi katika kujadili udhaifu badala ya kujadili namna ya kuboresha hali.       (alama 2× 1= 2)
  5. Wito wa aya ya mwisho
    Tuyachunguze mambo yaliyotuangusha na kuketi chini kuyajadili wazi, tukemeane na kurekebishana bila hofu.      (2×1= 2)
  6. Methali zinazohusiana na aya mbili za mwisho
    1. Umoja ni nguvu, utengano ni udhaifu
    2. Jifya moja haliinjiki chungu          (2 × 1 = 2)
  7.  
    1. kukidhi haja  - kutosheleza mahitaji / timiza matakwa
    2. kiu ya maendeleo – uchu wa kuwa na maendeleo / haja
    3. Tunyosheane vidole usoni – tukemeane / tuonyane        (3 ×1 = 3)

MUHTASARI

  1. Changamoto zinazoikumba lugha ya kiswahili kama lugha rasmi.
    • Lugha ya kiswahili kushindania nafasi sawa na ile ya kiingereza katika shughuli za kikazi.
    • Lugha ya Kiswahili itachukua nafasi ipi na kiingereza nacho kichukue ipi.
    • Kiwango cha maandalizi ya wananchi katika kuyapokea mabadiliko hay
    • Kufanyika kwa uandishi wa vitabu zaidi vya Kiswahili
    • Mtazamo hasi wa wananchi kuwa kiswahili ni lugha ngumu
    • Utoaji wa nafasi finyu kwa lugha ya Kiswahili miongoni mwa wazungummzaji ambao huzionea lugha za kigeni fahari
    • Kuharibiwa kwa Kiswahili na sheng au lugha za kienyeji
      Hoja    6 × 1 = alama 1 mtiririko =7
  2. Namna ya kuimarisha matumizi ya Kiswahili nchini
    • Watunga sera kueleza kinagaubaga mawanda ya matumizi ya lugha hizi mbili kazini.
    • Watumishi wa umma wapewe mafunzo maalumu kuhusu mbinu za mawasiliano katika Kiswahili
    • Vyuo vikuu na taasisi za mafunzo kuwaandaa wanafunzi wao wapya kuhusu mahitaji mapya ya kikatiba
    • Wanaohusika na utekelezaji wa sera wapate mafunzo kutoka kwa wataalamu wa Kiswahili
    • Kuandikiwa kwa vitabu zaidi vitakavyofunza mbinu za mawasiliano.
    • Wananchi wahimizwe kukionea fahari Kiswahili, wakipende na kukielewa
    • Viongozi wawe vielelezo kwa kukizungumza Kiswahili sanifu .
    • Viongozi wapewe kipaumbele katika kufunzwa kwa Kiswahili
      Hoja 7 × 1 = 7 Utiririko1        Jumla   alama 8

MATUMIZI YA LUGHA

  1. Taja sauti mbili za nazali.  (Al 2)
    • m/n/,ny/,/ng’/ (2x1=2)
  2. Taja aina mbili za mofimu na utolee mfano mmoja mmoja (al 2)
    • Mofimu huru- mama, kuku,kaka,kalamu
    • Mofimu tegemezi- moto, kitabu, analima (2x1=2)
  3. Tunga sentensi yenye kitenzi kishirikishi kipungufu (al 2)
    1. mtoto huyu ni mtiifu
    2. kitabu kile ndicho cha mwanafunzi (2x1=2)
  4. Tunga sentensi moja ukitumia  kihisishi na nomino maalum (al 2)
    Lo!Juma ni hodari katika kandanda
  5. Eleza maana ya chagizo na utunge sentensi moja kuonyesha maana yake (al2)
    1. chagizo ni maneno yanayochukua nafasi ya kielezi
    2. wageni wetu wanawasili kesho asubuhi
  6. Tumia “amba” rejeshi katika sentensi ifuatayo  (al 2)
    Mchezaji ninayempenda ni Messi
    • Mchezaji ambaye napenda ni Messi
  7. Yakinisha sentensi ifuatayo. (al 2)
    Asingepigiwa kura, asingekuwa rais wa Kenya.
    • Angepigiwa kura, angekuwa rais wa Kenya (al 2)
  8. Unda nomino kutokana na vitenzi vifuatavyo
    1. Tafakari – kutafakari, tafakuri
    2. Sujudu – kusujudu  (2x1=2), sajada
  9. Badilisha sentensi ifuatayo iwe katika hali ya kuamuru katika wingi (al. 2)
    Njoo hapa      njooni hapa!
  10. Andika katika msemo wa taarifa
    “Naapa ya kwamba nitatumikia wananchi wa Kenya na nitakuwa mwaminifu,” Rais mteule alisema (al 2)
    • Rais mteule aliapa kwamba angetumikia wananchi wa Kenya na angekuwa mwaminifu
  11. Onyesha vishazi katika sentensi ifuatayo (al2)
    • Uchaguzi uliofanywa nchini Kenya  - kishazi tegemezi
    • ulikuwa wa amani – kishazi huru
  12. Bainisha aina za shamirisho katika sentensi . Shule nzuri ilijengewa wanafunzi kwa matofali (al 3)
    shule nzuri ilijengewa wanafunzi kwa matofali
    • shule – shamilisho kipozi
    • wanafunzi – shamirisho kitondo
    • matofali - Ala
  13. Changanua sentensi ifuatayo ukitumia jedwali (al 4)
    Walimu shupavu walifunza vizuri lakini wanafunzi hawakupita mtihani
                                                                                                  S    
                                    S1    U                                         S2  
                       KN                      KT      KN                         KT 
     N  V  T  E    N  T  N
     walimu  shupavu  walifunza  vizuri  lakini  wanafunzi  hawakupita  mtihani
  14. Eleza sifa mbili za sentensi ambatano na utoe mfano mmoja (al 3)
    • huwa sentensi mbili sahihi
    • huwa na kiunganishi
    • huwa na mawazo mawili
      mf: mama alifua nguo kisha akapika chakula
      mtoto huyu ni mtiifu lakini huyu ni mtukutu
  15. Eleza matumizi tofauti ya kiambishi ‘ni’ katika sentensi ifuatayo (al 2)
    Nitasoma kwa bidii shuleni
    Nafsi ya kwanza                kielezi cha umoja
    umoja
  16. Tunga sentensi moja ukitumia neon ‘gani’ kama  (al 2)
    1. Kiwakilishi – Gani anatuzwa
    2. Kivumishi – Mwanafunzi gani anatuzwa
  17. Tunga sentensi ukitumia kitenzi ‘la’ katika hali ya kutendesha (al 2)
    • mama alimlisha motto chakula

ISIMU JAMII (al 10)

“Karibu wageni karibuni
Come and learn with us lugha ya Kiswahili
Nyote mtabenefit sana”
“Kwa nini?”
“Kwa sababu it’s a national language”

Maswali 
  1. Lugha ngapi zimetumika katika muktadha hii? (al 2)
    • lugha mbili
  2. Mtindo wa kutumia lugha zaidi ya moja katika mazungumzo huitwaje? (al 2)
    • kuchanganya ndimi
  3. Mzungumzaji mwenye uwezo wa kutumia lugha zaidi moja anaitwaje? (al 2)
    • Bilinguo / uwili lugha
  4. Taja sababu za wazungumzaji kutumia lugha zaidi ya moja (al 4)
    • ili kueleweka vizuri
    • kukosa msamiati katika lugha moja
    • kuwa na umahiri katika lugha zote
    • kukosa umahiri katika lugha moja/au zote
    • Kutaka kujihusisha na kundi Fulani  (zozote 4)
Join our whatsapp group for latest updates

Download Kiswahili paper 2 Questions and Answers - Form 3 End Term 1 Exams 2023.


Tap Here to Download for 50/-




Why download?

  • ✔ To read offline at any time.
  • ✔ To Print at your convenience
  • ✔ Share Easily with Friends / Students


Get on WhatsApp Download as PDF
.
Subscribe now

access all the content at an affordable rate
or
Buy any individual paper or notes as a pdf via MPESA
and get it sent to you via WhatsApp

 

What does our community say about us?

Join our community on:

  • easyelimu app
  • Telegram
  • facebook page
  • twitter page
  • Pinterest