Kiswahili Paper 3 Questions and Answers - Form 3 End Term 2 Exams 2023

Share via Whatsapp
Maagizo
  • Jibu maswali yote.
  • Kila swali ni alama 20.
  • Majibu yote yaandikwe kwa lugha ya Kiswahili

Swali la kwanza-Fasihi simulizi (alama 20)

  1. Soma utungo ufuatayo kisha ujibu maswali

    Wajukuu wangu nina furaha isiyo na kifani kuchukua jukumu hili la kutoa nasaha zangu kwenu hasa wakati huu mnapojiandaa kufunga nikahi yenu. Ni jambo la kutia moyo kwangu kuona nasaba yetu inaendelea kupanuka na si hapa kijijini tu, bali imevuka mipaka ya nchi.

    Wajukuu wangu, ndoa ni asasi muhimu sana maishani mwa mwanadamu yeyote katika sehemu yoyote duniani. Ni asasi inayotukuzwa na kuenziwa na jamii nyingi .Hii ni kwa kuwa ndoa huwawezesha wawili kuungana na kuwa kitu kimoja ili kutegemeana na kuondoa upweke  kama wahenga walivyosema ‘mtu pweke ni uvundo’.Wajukuu wangu nawapongeza kwa kuupa upweke kisogo.

    Wanangu, ulimwengu umebadilika .Sasa dunia imekuwa kijiji kimoja ambapo watu kutoka sehemu mbalimbali wanaingiliana. Huu ndio wanaouita utandarithi.Nyinyi ni wapenzi kutoka nchi mbili tofauti na mmekuwa kielelezo cha mabadiliko haya  duniani. Mmevunja vikwazo na vizuizi vya mipaka ya nchi.bara pamoja na utamaduni.Mmedhihirisha kuwa mke au anaweza kupatikana kutoka eneo lolote duniani mradi tu pawe na maelewano.

    Maharusi ,sasa ndio mnaanza safari.Mkondo huu wa kujenga nyumba ni mgumu ila mkivumiliana na kuelewana mtafaulu.Wengi wamefaulu .Mbona nyinyi msiweze?Changamoto kubwa kwenu sasa ni uwezo wa kuelekeza fikra zenu ili ziweze kuingia katika mkondo mmoja wa mawazo na uamuzi.Itabidi mtupilie ubinafsi kando na kuwa lolote mtakalokuwa mkitekeleza litakuwa ni uamuzi wa pamoja.

    Mnapaswa kuelewana na kila mmoja kukamia kumwelewa mwenzake.Ni muhimu kuwa wavumilivu na kila mmoja kukamia kumwelewa mwenzake.Ni muhimu kila mmoja kujaribu kuuelewa utamaduni wa mwenzake  kwani utamaduni humjenga mtu na huchangia sana maamuzi yoyote anayofanya maishani.Ni lazima ung’amue kwamba huwezi kumbadilisha mwenzio kiutamaduni kwa ghafla  kwani kila mmoja ana dini, imani, ada,,chakula anachokitukuza ,mtazamo na falsafa fulani kuhusu maisha .Tofauti ya asili zenu zisiwe sababu za kuisambaratisha ndoa yenu bali ziwe msingi thabiti wa mapenzi na ndoa yenu!

    Maswali
    1. Kwa kutolea mifano tambua kipera cha utungo huu. (alama 2)
    2. Eleza changamoto zinazowakabili wanandoa hawa ? (alama 5)
    3. Kwa nini msimulizi anasema ndoa ni asasi muhimu katika maisha ya binadamu. (alama 2)
    4. Je,msemaji ni nani katika usimulizi huu?        (alama 1)
    5. Kulingana na utungo huu tambua umuhimu wa utamaduni kwa binadamu.     (alama 2)
    6. Kwa kutolea hoja nane onyesha umuhimu wa kipera hiki katika jamii.            (alama 8)
  2. USHAIRI
    Soma shairi lifuatalo kisha ujibu maswali yanayofuata.

    Angajiita mzuri, umbo lake limewanda
    Angatiwa na uturi, hakosi katu kuvunda
    Mpe ubani fakiri,ahadi ataivunda
    Hajifichi mnafiki ,sifaze humfichuwa.

    Ja bozi kule jangwani, juhudi kujisitiri
    Nyeupe kanzu mwilini, masafa ni ya shubiri
    Ni mwongo tangu zamani, hatendi kwa tafakuri
    Hajifichi mnafiki, sifaze hufichuwa.
    Kujikalifu usende ,kusaka na ithibati
    Bahati kama mtende, usiazimu kunuti
    Amana mpe alinde, hafikishi zamarati
    Hajifichi mnafiki ,sifaze humfichuwa.

    Wa wazi nduli heri, kuliko mpulizaji
    Hutubu akaghairi ,kanama udanganyaji
    Zandiki likashamiri, halina muokoaji
    Hajifichi mnafiki, sifaze hufichuwa.

    Duniya tunamoishi ,madhara tunayopata
    Katika aushi yetu ,shiya wa bukurata
    Mnafiki ni mzushi,yakizidi huyabwata
    Hajifichi mnafiki, sifaze hufichuwa.

    Manani wetu wahidi, aso katu mshirika
    Hutujaliya weledi, pasi rika na tabaka
    Tukatambuwa fisadi, tusipate kudhurika
    Hajifichi mnafiki, sifaze hufichuwa.

    Maswali
    1. Lipe kichwa mwafaka shairi hili.    (alama 1)
    2. Onyesha dhamira ya mshairi wa shairi hili. (alama 2)
    3. Onyesha muundo wa shairi hili. (alama 4)
    4. Tambua sifa za nafsinenewa.  (alama 4)
    5. Toa mfano wa usambamba katika shairi hili. (alama 1)
    6. Andika ubeti wa kwanza kwa lugha ya tutumbi. (alama 4)
    7. Onyesha mbinu  nne alizotumia malenga ili kutosheleza mahitaji ya kiarudhi katika shairi hili. (alama 4)
  3. TAMTHILIA-BEMBEA YA MAISHA na Timothy Arege
    “Huko ndiko kuvumilia hasa. Tazama faraja ilivyoalika sasa.”
    1. Weka dondoo hili katika muktadha. (alama 4)
    2. Eleza sifa na umuhimu wa mhusika huyu katika Tamthilia ya Bembea ya maisha.  (alama 6)
    3. Kwa kutolea hoja kumi onyesha jinsi faraja ilivyoalika katika maisha ya mlengwa wa maneno kwenye dondoo. (alama 10)
  4. HADITHI FUPI-MAPAMBAZUKO YA MACHWEO NA HADITHI NYINGINE
    “Kwa nini nisilipe ?Mnadhani mashaibu kama sisi ni mafukara hohehahe hatuna pesa mfukoni ?Hebu twende naona dereva yule ana haraka sana.Mkimbize!”
    1. Tambua muktadha wa dondoo hili. (alama 4)
    2. Onyesha mbinu za kimtindo zinazojitokeza katika dondoo hili. (alama 4)
    3. Msemaji wa dondoo hili ana sifa gani? (alama 6)
    4. Migogoro tofauti tofauti imeshuhudiwa katika hadithi hii .Thibitisha.      (alama 6)

MARKING SCHEME

  1. Swali la kwanza - Fasihi simulizi
    1. Kwa kutolea mifano tambua kipera cha utungo huu. (alama 2)
      • Mawaidha-Kuwapa nasaha
    2. Eleza changamoto zinazowakabili wanandoa hawa ? (alama 5)
      • Kila mmoja anatoka katika nchi na bara tofauti
        Na kuna;
      • Tofauti katika utamaduni
      • Tofauti za kidini
      • Tofauti za Imani
      • Tofauti za ada
      • Tofauti za vyakula
      • Mitazamo na falsafa tofauti kuhusu maisha
        Hoja zozote 5*1=5
    3. Kwa nini msimulizi anasema ndoa ni asasi muhimu katika maisha ya binadamu. (alama 2)
      • Ukoo huendelea kupanuka
      • Huwaunganisha wawili na kuwa kitu kimoja ili kutegemeana na kuondoleana upweke
    4. Je,msemaji ni nani katika usimulizi huu? (alama 1)
      • Ni nyanya /babu wa mmoja wa wanandoa
    5. Kulingana na utungo huu tambua umuhimu wa utamaduni kwa binadamu.     (alama 2)
      • Humjenga mtu na huchangia kwa maamuzi yoyote anayofanya mja maishani
    6. Kwa kutolea hoja nane onyesha umuhimu wa kipera hiki katika jamii.         (alama 8)
      • Hupitisha maadili ya jamii kwa wale wanaoshauriwa
      • Kuelimisha jamii
      • Kuonya dhidi ya kujihusisha na tabia hasi
      • Huwapa vijana mbinuishi za kukabiliana na changamoto za maisha
      • Hukuza uwezo wa kufikiri
      • Hufariji na kuliwaza hasa wale wamekumbwa na mikasa
      • Ni chombo cha kuwapa wanajamii matumaini
      • Huhifadhi na kuendeleza utamaduni wa jamii
      • Ni njia ya kupata riziki hasa kwa wataalamu wa ushauri nasaha
        Za kwanza 8*1=8
  2. USHAIRI
    1. Lipe kichwa mwafaka shairi hili. (alama 1)
      • Mnafiki hajifichi ,hufichua sifa zake
        (Kadiria jibu la mwanafunzi)
    2. Onyesha dhamira ya mshairi wa shairi hili. (alama 2)
      • Kufichua sifa tofauti tofauti za mtu mnafiki
    3. Onyesha muundo wa shairi hili. (alama 4)
      • Shairi hili lina’
      • Mishororo mine katika kila ubeti
      • Lina vipande viwili katika kila mshororo
      • Vina vya kati na vya mwisho vinabadilika badilika kutoka ubeti mmoja hadi mwingine
      • Lina kibwagizo-Hajifichi mnafiki.sifaze hufichuwa
    4. Tambua sifa za nafsinenewa. (alama 4)
      • mvunja ahadi-ahadi ataivunda
      • ni mwongo-ni mwongo tangu zamani
      • hutelekeza majukumu-hafikishi zamarati
      • Ni mzushi-mnafiki ni mzushi
    5. Toa mfano wa usambamba katika shairi hili. (alama 1)
      • hakosi katu kuvunda
      • ahadi ataivunda
    6. Andika ubeti wa kwanza kwa lugha ya tutumbi. (alama 4)
      • Mnafiki hata ajitambulishe kama mtu mzuri na ajipake marashi bado atakuwa mtu mbaya tu.Hata umfukie ubani bado ahadi ataivunya tu.Kwani mnafiki hajifichi sifa zake ndizo humfichua.
    7. Onyesha mbinu  nne alizotumia malenga ili kutosheleza mahitaji ya kiarudhi katika shairi hili. (alama 4)
      • inkisari-usende-usiende, sifaze-sifa  zake
      • lahaja-kuvunda-kuvunja
      • kuboronga sarufi-hajifchi mnafiki-mnafiki hajifichi
      • tabdila-humfichuwa-humfichua, duniya-dunia
  3. TAMTHILIA-BEMBEA YA MAISHA na Timothy Arege
    “Huko ndiko kuvumilia hasa. Tazama faraja ilivyoalika sasa.”
    1. Weka dondoo hili katika muktadha. (alama 4)
      • Maneno ya Dina
      • Kwa Sara
      • Wakiwa nyumbani kwa Sara jikoni
      • Sara alikuwa amemtumia wito Dina aende amsaidie kupika
    2. Eleza sifa na umuhimu wa msemaji  huyu katika Tamthilia ya Bembea ya maisha. (alama 6)
      • Mwenye huruma-anamhurumia Sara jinsi anavyouguza ugonjwa wake
      • Mwenye ujirani mwema-anakuwa tayari kumsaidia Sara kama jirani wake
      • Mwenye roho safi-hamwonei wivu Sara kwa kufanikiwa kwa watoto wake
      • Mwenye mapenzi ya dhati-Hakatai wito wa Sara
      • Ana kumbukumbu nzuri-anakumbuka masaibu ya Sara katika ndoa yake
      • Ana mlahaka mzuri na mtoto wake Kiwa –anakuja kumjulia hali
        Umuhimu
      • Ni kielelezo cha majirani wema katika jamii
      • Mwandishi amemtumia kutuonyesha masaibu aliyopitia Sara katika ndoa yake
      • Anaendeleza ploti-mazungumzo yake na Sara yabadilisha mkondo wa matukio katika hadithi  tunajua   kuwa Sara ataenda mjini kwa sababu ya matibabu
    3. Kwa kutolea hoja kumi onyesha jinsi faraja ilivyoalika katika maisha ya  msemewa maneno kwenye dondoo.
      (alama 10)
      • Sara na Yona wanajaliwa watoto watatu wa kike baada ya muda
      • Yona anabaki kwa ndoa licha ya shinikizo kutoka kwa wanajamii aoe mke mwingine ili ampe mtoto kijana
      • Sara ana jirani kama Dina ambaye anamsaidia kila anapolemewa
      • Sara anamsidia Yona kuwasomesha watoto wao alipopoteza kazi ya ualimu
      • Watoto wao wanahitimu masomo yao hadi chuo kikuu
      • Neema anaolewa na bwana anayempenda na kumjali-Bunju
      • Ndoa ya Bunju na Neema inawapa Sara na Yona wajukuu-Lime na Mina
      • Sara anakuja kuchukuliwa kwa gari na Neema kumpeleka mjini kwa sababu ya matibabu
      • Mjini Sara anapelekwa kwa Hospitali nzuri ya wataalamu wanaoshughulikia ugonjwa wake vilivyo
      • Neema na Bunju wamewajengea Sara na Yona nyumba
      • Neema anampa babake Yona pesa za dawa na za masurufu
      • Kijijini jina la Neema limeenea kwa sifa ya kuwa mja wa kwanza kuendesha gari kijijini
      • Neema anawanunulia wazazi wake kochi mpya
      • Neema anawanunuliwa wazazi wake jiko la gesi
      • Yona anaanza kumjali mkewe Sara kwa kumpikia kiamsha kinywa
        Za kwanza 10*1=10
  4. HADITHI FUPI-MAPAMBAZUKO YA MACHWEO NA HADITHI NYINGINE
    “Kwa nini nisilipe ?Mnadhani mashaibu kama sisi ni mafukara hohehahe hatuna pesa mfukoni ?Hebu twende naona dereva yule ana haraka sana.Mkimbize!”
    1. Tambua muktadha wa dondoo hili. (alama 4)
      • Maneno ya Mzee Makucha
      • Kwa dereva wa teksi
      • Akiwa barabarani anakouzia bidhaa zake
      • Alikuwa anataka kumfuata gari la Bwana Makutwa ili amdadisi anakokuwa anakwenda.
    2. Onyesha mbinu za kimtindo zinazojitokeza katika dondoo hili. (alama 4)
      • Swali balagha-Kwa nini nisilipe?
      • Hohehahe-msemo-maskini kabisa
      • Dereva-utohozi
      • Nidaa-mkimbize!
    3. Msemaji wa dondoo hili ana sifa gani? (alama 6)
      • Mwenye bidii –baada ya kufutwa kazi anaanza kuuchuza vitafunio barabarani
      • Ni mpelelezi-anapanda teksi na kufuata gari la Makutwa kumpeleleza anakopeleka vijana
      • Ni mazalendo-anawaita polisi kuwaokoa vijana wanaogandamizwa na Makutwa ndani ya migodi
      • Ni mjanja-anafaulu kuingia katika pango la mgodi licha ya kuwa na walinzi waliomzuia
      • Ni mwerevu-Walinzi waliokuwa wanawahangaisha vijana waliobwagwa na teksi anaingia ndani akidai alikuwa anamtafuta Makutwa na kwa sababu alimkosa sasa alitaka kuondoka ilhali ndio alikuwa anaenda kuwapasha polisi.
      • Mwepesi wa kukasirika-mkewe anapomzungumzia kuhusu Makutwa anamjibu kwa hasira.Maneno ya Makutwa kumhusu mwanao Riziki pia yanamkera
        Zozote6*1=6
    4. Migogoro tofauti tofauti imeshuhudiwa katika hadithi hii .Thibitisha.         (alama 6)
      • Mgogoro kati ya marafiki-Makutwa na Makucha-Makucha anapofutwa kazi na Makutwa kustaafishwa kila mtu anaingilia biashara tofauti-Makuucha anachuuza vitafunio barabarani kazi ambayo anaidhihaki Makutwa na kusbabisha chuki kati yao.
      • Makucha anakuwa na mgogoro wa nafsi baada ya kufutwa kazi katika shirika la reli nchini  .Anajaribu kutafuta haki mahakamani lakini anakosa kufua dafu.
      • Bi. Macheo anajipata katika mgogoro na mumewe kuhusiana na Makutwa-Hapendi Makutwa anavyomfanyia dhihaka mumewe kila mara na anataka kuukomesha uhusiano  wao.
      • Macheo pia ana mgogoro kuhusu tabia ya Makutwa kuwabeba vijana katika gari lake ilhali yeye ni mzee.
      • Kuna mgogoro baina ya Makucha na Makutwa kutokana na Makutwa kutumia vijana vibaya ili kujitajirisha
      • Mgogoro unaimarika Makucha anapojua kazi ambayo Makutwa hufanya ya kuwatumikisha vijana katika mgodi wa kutafuta vito.Anaamua kwenda kuwaita polisi ambao wanaenda kwenye mgodi huo kumkamata Makutwa. Makutwa anamlaumu kwa kumwita rafiki wa uongo.
      • Makutwa anajipata kwa mgogoro wa kisheria-anaposhikwa kwa kosa la kuwatesa vijana katika migodi
        Hoja zozote 6*1=6
Join our whatsapp group for latest updates

Download Kiswahili Paper 3 Questions and Answers - Form 3 End Term 2 Exams 2023.


Tap Here to Download for 50/-




Why download?

  • ✔ To read offline at any time.
  • ✔ To Print at your convenience
  • ✔ Share Easily with Friends / Students


Get on WhatsApp Download as PDF
.
Subscribe now

access all the content at an affordable rate
or
Buy any individual paper or notes as a pdf via MPESA
and get it sent to you via WhatsApp

 

What does our community say about us?

Join our community on:

  • easyelimu app
  • Telegram
  • facebook page
  • twitter page
  • Pinterest