Kiswahili Paper 3 Questions and Answers - Form 4 Mid Term 2 Exams 2021

Share via Whatsapp

KISWAHILI
KARATASI YA 3
KIADTO CHA NNE
MTIHANI WA KATI YA MUHULA

MAAGIZO

 • Andika jina lako, nambari ya mtihani na tarehe katika karatasi ya majibu.
 • Karatasi hii ina sehemu tano: A, B, C, D na E.
 • Jibu maswali manne pekee. Kila swali lina alama ishirini.
 • Swali la kwanza ni la lazima.
 • Chagua maswali mengine yoyote matatu kutoka sehemu zilizosalia; B, C, D ama E.
 • Usijibu maswali mawili kutoka sehemu moja.
 • Majibu yote yaandikwe kwa Kiswahili katika karatasi ya majibu uliyopewa.

MASWALI

 1. SEHUMU YA A: TAMTHILIA: KIGOGO (Pauline Kea)
  1. “Ni laghai siwaamini. Wanasema wanakwenda huku na mara…”
   1. Eleza muktadha wa dondoo hili. (Alama 4)
   2. Eleza mbinu ya lugha iliyotumiwa katika dondoo hili. (Alama 2)
   3. Eleza sifa na umuhimu wa mzungumzaji. (Alama 6)
   4. Fafanua jinsi wanaorejelewa na mzungumzaji walivyo laghai. (Alama 10)

 2. SEHEMU YA B: RIWAYA: CHOZI LA HERI (Assumpta K. Matei)
  Jibu swali la Pili au la Tatu
  1. “Watu husema kuwa binadamu hawawi sawa ila kifoni…”
   1. Eleza muktadha wa maneno haya. (alalama 4)
   2. Tambua mbinu moja ya lugha iliyotumiwa katika dondoo hili. (alama 2)
   3. Eleza sifa na umuhimu wa mzungumzaji wa maneno haya. (alama 6)
   4. Thibitisha kuwa hakuna usawa baina ya wanadamu. (alama 8)

    Au
  2. Jadili nafasi ya sehemu zifuatazo katika riwaya ya Chozi la Hari:
   1. Hotuba (alama 10)
   2. Uozo katika jamii (alama 10)

 3. SEHEMU YA C: HADITHI FUPI: TUMBO LISILOSHIBA NA HADITHI NYINGINE (Alifa Chokocho na Dumu Kayanda- Wahariri)
  Jibu swali la Nne ama la Tano
  NDOTO YA MASHAKA
  1.  “Sasa nimechoka mja. Nimechoka hata naradua kufa kuliko kuishi.”
   1. Eleza muktadha wa dondoo hili. (alama 4)
   2. Taja mbinu mbili za lugha katika dondoo hili. (alama 4)
   3. Mzungumzaji alikuwa na haki ya kuradua kufa. Thibitisha. (alama 12)

    Au
  2. Ukirejelea hadithi zozote nne katika diwani ya Tumbo Lisiloshiba na Hadithi Nyingine, eleza jinsi maudhui ya Mapenzi na ndoa yanavyojitokeza (alama 20)

 4. SEHEMU YA D
  USHAIRI
  Jibu swali la sita ama la saba
  1. Soma shairi lifuatalo kasha ujibu masuali

   Naogopa, kukupa wangu mtima, sitaki mie nilie
   Naogopa, kutoa yangu kalima, eti wewe utulie
   Naogopa, ninashindwa kusimama, wewe pete unitie
   Naogopa, wanaume wanauma, ja panya wapulizie.
   Naogopa, kwita wako mama mama, nami anikaripie
   Naogopa, sipendi nyingi dhuluma, za wanaume nilie
   Naogopa, kushinda nimeinama, goti mume nipigie
   Naogopa, za mkemwenza hujuma, matusi anipatie.
   Naogopa, kwita wako mama mama, nami anikaripie
   Naogopa, sipendi nyingi dhuluma, za wanaume nilie
   Naogopa, kushinda nimeinama, goti mume nipigie
   Naogopa, za mkemwenza hujuma, matusi anipatie.
   Naogopa, uchungu ukiniuma, mwana nikakuzalie
   Naogopa, kupigwa kama ngoma, ndiposa nikatulie
   Naogopa, kila kitu kunisoma, ndo hela unipatie
   Naogopa, kuitwa mwizi wa sima, ila nikuandalie.
   Naogopa, dadazo kuwaandama, udaku wakanitie
   Naogopa, kuuleta uhasama, mimi mnipiganie
   Naogopa, koritini kusimama, mali tukashindanie
   Naogopa, kumwaga wenu mtama, kuku niwamiminie,
   Naogopa, naogopa ninasema, yabidi uvumilie
   Naogopa, nawe babu kusimama, eti ndoa niingie
   Naogopa, ndoto zangu kuzizima, hili doa nijitie
   Naogopa, taa yangu kuizima, mwingine jitafutie.
   (Meja S. Bukachi- Uketo wa Ushairi uk 24)

   MASWALI
   1. Lipe shairi hili anwani mwafaka. (Alama 1)
   2. Eleza dhamira ya mtunzi wa shairi hili. (Alama 1)
   3. Nani nafsi nenewa katika shairi hili? (Alama 1)
   4. Taja tamathali za lugha zilizotumika katika shairi hili. (Alama 2)
   5. Fafanua uhuru wa ushairi alioutumia malenga. (Alama 2)
   6. Weka shairi hili katika bahari mbalimbali. (Alama 3)
   7. Andika ubeti wa tatu kwa lugha nathari. (Alama 4)
   8. Kwa nini nafsi neni anasita kuchukua hatua? (alama 4)
   9. Vifungu vifuatavyo vina maana gani katika shairi? (alama 2)
    1. Taa yangu kuizima
    2.  Dhuluma

     Au

  2. Soma shairi lifuatalo kisha ujibu maswali

   Ee mpwa wangu,
   Kwetu hakuna muoga,
   Uoga ukikufikia, huenda ni wa akina mamayo,
   Fahali tulichinja ili uwe mwanamume,
   Eewe mpwa wangu, kisu kikali ajabu!
   Iwapo utatingisha kichwa,
   Uhamie kwa wasiotahiri.
   Wanaume wa mbari yetu,
   Si waoga wa kisu,
   Wao hukatwa kuanzia macheo hadi machweo,
   Wewe ndiye wa kwanza,
   Iwapo utashindwa,
   Wasichana wote,
   Watakucheka,
   Ubaki msununu,
   Simama jiwe liwe juu,
   Ndege zote ziangamie.
   Wanaume wa mbari yetu,
   Si waoga wa kisu,
   Wao hukatwa kuanzia macheo hadi machweo,
   Wewe ndiye wa kwanza,
   Iwapo utashindwa,
   Wasichana wote,
   Watakucheka,
   Ubaki msununu,
   Simama jiwe liwe juu,
   Ndege zote ziangamie.
   Simu nimeipokea,
   Ngariba alilala jikoni,
   Visu ametia makali,
   Wewe ndiye wangojewa,
   Hadharani utasimama,
   Macho yote yawe kwako,
   Iwapo haustahimili kisu,
   Jiuzulu sasa mpwa wangu,
   Hakika sasa mpwa wangu,
   Hakika tutakusamehe, mwaka kesho unakuja.
   Asubuhi ndio hii,
   Mama mtoto aamushwe,
   Upweke ni uvundo,
   Iwapo utatikisa kichwa,
   Iwapo wewe ni mume,
   Kabiliana na kisu kikali,
   Hakika ni kikali!
   Kweli ni kikali!
   Wengi wasema ni kikali!
   Fika huko uone ukali!
   Mbuzi utapata,
   Na hata shamba la mahindi,
   Simama imara,
   Usiende kwa wasiotahiri

   Maswali
   1. Hili ni shairi la aina gani? Thibitisha. (alama 2)
   2. Ni nani anayeimba shairi hili na analiimba kwa nani ? (alama 2)
   3. Toa ithibati kwenye shairi hili kuthibitisha kuwa msimulizi ana taasubi ya kiume (alama 2)
   4. Taja kwa kutolea mifano mbinu zozote nne za uandishi katika shairi hili (alama 4)
   5. Taja shughuli zozote mbili za kiuchumi za jamii inayorejelewa katika shairi hili (alama 2)
   6. Eleza kwa mifano, uhuru wa kishairi katika shairi hili (alama 4)
   7. Msamiati ufuatao umetumika kwa maana gani katika shairi hili? (alama 4)
    1. Mbari
    2. Msununu
    3. Ngariba
    4. Uvundo

 5. SEHEMU YA E: FASIHI SIMULIZI
  1. Soma utungo ufatao kisha ujibu maswali

   Ikiwa kweli wewe ni mkazamwanangu,
   Nami ndiye niliompa uhai mwana unoringia,
   Anokufanya upite ukinitemea mate,
   Chakula kuninyima, wajukuu kunikataza ushirika,
   Miungu na waone chozi langu, wasikie kilio changu,
   Mizimu na waone uchungu wangu,
   Radhi zao wasiwahi kukupa,
   Laana wakumiminie,
   Uje kulizwa mara mia na wanao,
   Usiwahi kufurahia hata siku moja pato lao,
   Watalokupa likuletee simanzi badala ya furaha,
   Wakazawanao wasikuuguze katika utu uzima wako!
   (Kutoka: Assumpta K. Matei- Fani ya Fasihi Simulizi, uk 145)

   Maswali
   1. Tambua kipera hiki cha fasihi simulizi (alama 2)
   2. Jinsia ya nafsi neni ni gani? (alama 2)
   3. Eleza sifa zozote sita za kipera hiki cha fasihi simulizi. (alama 6)
   4. Fafanua umuhimu wa kipera ulichokitaja hapo juu katika jamii. (alama 4)
   5. Fafanua njia sita jinsi jamii ya kisasa inavyojaribu kuendeleza fasihi simulizi. (alama 6)

MWONGOZO WA KUSAHIHISHIA

 1. SEHUMU YA A: TAMTHILIA: KIGOGO (Pauline Kea)
  1.  “Ni laghai siwaamini. Wanasema wanakwenda huku na mara…”
   1. Eleza muktadha wa dondoo hili. (Alama 4)
    • Haya ni maneno ya Majoka. Anamwambia Babu anapokuwa amezimia. Yupo katika chumba cha wagonjwa. Majoka analalamika kuwa chombo kinaenda kinyume na matarajio yake. Babu anamtaka Majoka asilalamike kwani yeye ni mmoja wa marubani. (4×1= 4)
   2. Eleza mbinu ya lugha iliyotumiwa katika dondoo hili. (Alama 2)
    • Kinaya- Majoka analalamika kuwa hawapendi marubani ilhali yeye ni mmojawapo wa marubani. (1×2= 2) lazima maelezo yawe sahihi ndiposa mtahiniwa apate alama zote mbili. Moja ya kutaja na moja ya kueleza. Bila maelezo sahihi kwa jibu sahihi tuza 0
   3. Eleza sifa na umuhimu wa mzungumzaji. (Alama 6)

    • Sifa za Majoka
     1. Ni Katili. Anawaua wapinzani wake. Anamwangamiza Jabali na chama chake cha Mwenge kwa kuhofia upinzani. Aidha, anapanga njama za uuaji wa Wanasagamoyo wengine, kama Tunu, Chopi na hata Sudi (uk 34).
     2. Mwepesi wa kushawishika. Anakubali bila kudadisi athari za ushauri mbovu wa Kenga kuwa wamwangamize Chopi. Aidha, anautumia ushauri wa Kenga wa kumnasa Ashua ili kulipa kisasi kwa Sudi aliyekataa kumchongea kinyago (uk 29).
     3. Ni mwingi wa tamaa. Ana tamaa kubwa ya mali. Ananyakua shamba la soko la Chapakazi ili aweze kujijengea hoteli kubwa ya kifahari. Ana mali mengi ikiwemo Majoka and Majoka Company, Majoka and Majoka Academy, Majoka and Majoka Mordern Resort na bado haridhiki.
     4. Ni mwenye uchu. Ana tamaa za kimwili. Anatamani kushiriki mapenzi na Ashua licha ya kuwa Ashua ameolewa naye mwenyewe ana mke (uk 29).
     5. Mwenye taasubi. Hawathamini wanawake. Anaamini kuwa mwanamke ni mwanamke tu. Anatishia kumchafua Husda.
     6. Ni fisadi. Ananyakua mashamba ya umma kwa manufaa yake mwenyewe. Anamgawia Kenga kipande cha shamba huko sokoni kwa kigezo kuwa anashirikiana vyema naye.
     7. Mkware/Mzinzi. Hamwamini mkewe tu. Anataka kushirikiana mapenzi na Ashua ambaye si mke wake wa ndoa (uk 28). (3×1= 3)
     8. Kila hoja ifafanuliwe ndiposa mtahiniwa atuzwe alama moja

    • Umuhimu wa Majoka
     1. Ni kielelezo cha viongozi wabaya na katili wanaowanyanyasa wananchi.
     2. Ametumiwa kupigia darubini viongozi wa mataifa huru ya Afrika na jinsi wanavyowanyanyasa wananchi kwa kufuata uongozi mbaya wa vibaraka wao.
     3. Ni kiwakilishi cha viongozi wanaokengeuka pindi tu baada ya kupewa uongozi na wananchi ili kukidhi tama zao. (3×1= 3)
     4. Hoja za umuhimu ziwe na ulinganifu fulani na sifa
   4. Fafanua jinsi wanaorejelewa na mzungumzaji walivyo laghai. (Alama 10)
    • Wanaoreewa ni viongozi.
    • Viongozi hawa ni laghai kwani:
     1. Hawahifadhi mazingira. Maji machafu (uchafuzi wa mazingira) yalipita mtaroni na kueneza harufu mbaya kila mahali bila uongozi wa Sagamoyo kuliona hili kuwa tatizo (uk 2).
     2. Wanahatarisha maisha ya wananchi. Soko la Chapakazi limebadilishwa na kufanywa uwanja wa kumwagia kemikali (uk 2).
     3. Wanawadhulumu wafanyabiashara. Wafanyabiashara wanahangaishwa na wanaosanya ushuru kwa kuwaitisha kitu kidogo na wengine kitu kikubwa (uk 2–3).
     4. Hawajali maendeleo ya kesho. Serikali kutangaza mwezi mzima wa kusherehekea uhuru bila watu kufanya kazi ilhali haijali watakachokula watu (uk 4).
     5. Hawana sera bora za maendeleo. Serikali ya Sagamoyo haina mipango maridhawa ya kimaendeleo. Majoka anamiliki kampuni kubwa ya sumu ya nyoka badala ya miradi muhimu (uk 4).
     6. Wanaruhusu na kuendeleza ufisadi. Kuna ufisadi unaomfanya Asiya kupata kandarasi ya uokaji keki ya uhuru kwa kujuana na Husda bali si kwa kufuzu na kufaulu (uk 7).
     7. Wanaendeleza udikteta. Utawala wa Sagamoyo ni wa kimabavu. Kenga anamlazimisha Sudi amchongee Majoka kinyago cha Ngao licha ya kujua kuwa uongozi wa Majoka ni wa udhalimu (uk 9).
     8. Wanatazama mambo nchini yakiendelea kuharibika. Kombe, mshiriki wa karibu wa Kenga anakiri kuwa mambo yameenda kombo Sagamoyo (uk 15).
     9. Hawajali maslahi ya wananchi. Uongozi unafunga soko la Chapakazi. Soko hili ndilo kitegauchumi pekee kwa Wanasagamoyo (uk 25).Wanawachochea wananchi kuandamana. Kuna maandamano ya mara kwa mara na yasiyotatuliwa katika jimbo la Sagamoyo, wanachi wanapigania haki zao.
     10. Wanaendeleza matumizi mabaya ya asasi za kijamii. Majoka anawatumia polisi wake vibaya ili kujidumisha uongozini. Polisi wanawanyanyasa na kuwadhulumu wananchi bila Majoka kujali.
     11. Wana ubinafsi mwingi. Sagamoyo kuna uongozi wa ubinafsi. Majoka anataka kuendeleza ubinafsishaji wa uongozi wa Sagamoyio kwa kumtangaza rasmi Ngao Junior kuwa mrithi wake (uk37).
     12. Wanaendeleza unyakuzi wa ardhi. Kuna unyakuzi wa mali ya umma. Majoka analifunga soko na kuinyakua sehemu hiyo ili ajenge hoteli ya kifahari (uk 45). (10×1= 10)

      (Kila hoja ifafanuliwe kikamilifu)

 2. SEHEMU YA B: RIWAYA: CHOZI LA HERI (Assumpta K. Matei)
  Jibu swali la Pili ama la Tatu
  1. “Watu husema kuwa binadamu hawawi sawa ila kifoni…”
   1. Eleza muktadha wa maneno haya (alalama 4)
    • Haya ni maneno ya Kaizri. Anamwambia Ridhaa. Wapo katika Msitu wa Mamba. Ni baada ya kufurushwa kutoka Mlima wa Simba baada ya vita vya baada ya uchaguzi kuzuka. Anarejelea usawa kiasi uliokuwa ukionekana kuwepi pale kambini. (4×1= 4)
   2. Tambua mbinu moja ya lugha iliyotumiwa katika dondoo hili (alama 2)
    • Kinaya- watu hawawi sawa ila kifoni(1×2= 2)
   3. Eleza sifa na umuhimu wa mzungumzaji wa maneno haya (alama 6)
    • Sifa za Kaizari.
     1. Ni mwenye busara. Anaelewa kuwa hakuna usawa wakati wa kifo kati ya maskini na matajiri ikizingatiwa wanavyokufa na wanavyozikwa (uk 14- 15).
     2. Ni maskini. Matone mazito ya mvua yalianguka kwenye ngozi ya wanawe, Lime na Mwanaheri. Hana uwezo wa kuwasaidia. Hata tambara hana (uk 15- 16).
     3. Ni mcha Mungu. Anamshukuru Mungu kuwa wangali hai licha ya hali ngumu (uk 16).
     4. Mwenye huruma. Aliwahurumia vijana waliouwawa kwa risasi na polisi wa Penda Usugu Ujute (uk 24).
     5. Mzalendo. Aliihurumia nchi yake ambayo ilielekea kushindwa kuwashawishi watu wake kuelewa umuhimu wa usalama (uk 24- 24).
     6. Mwenye mapenzi ya dhati. Alijaribu sana kuwaokoa wanawe waliokuwa wakibakwa ila akashindwa (uk 25).
     7. Mwenye tahadhari. Siku za kwanza kambini hakuweza kutumia vyoo vya kupeperushwa (uk 29).
     8. Mshawishi. Aliwasihi wakimbizi wenzake kuchimba misala (long drop) (uk 29). (3×1= 3)
     9. Kila sifa ifafanuliwe. Sifa zisianze kwa vinyume kama: hana utu, si mwenye tahadhari n.k.
    • Umuhimu wa Kaizari
     1. Anawakilisha watu wenye busara katika jamii.
     2. Ametumiwa kuonyesha matatizo wanayokumbana nayo wakimbizi.
     3. Anawakilisha athari zinazotokana na vita vya kikabila.
     4. Ametumiwa kuwajenga wahusika wengine kama Ridhaa. (3×1= 3)
   4. Thibitisha kuwa hakuna usawa baina ya wanadamu (alama 8)
    • Sheria za kikoloni zilimpa mzungu kibali cha kumiliki mashamba katika sehemu zilizotoa mazao na umilikaji wa ardhi na Waafrika sehemu hizi kupigwa marufuku (uk 7).
    • Hata katika kifo hamna usawa. Kuna wanaokufa wakipepewa na wauguzi katika zahanati za kijijini. Wengine hulala maumivu yao yakiwa yamefishwa ganzi kwenye hospitali za kifahari (uk 14).
    • Pia kuna tofauti katika mitindo ya mazishi ya matajiri na maskini. Matajiri huvishwa mavazi ya kifahari tofauti na maskini (uk 15).
    • Mwalimu aliwaambia kina Tila kuwa utawala huteuliwa maksudi kuendeleza mfumo uliopo wa kiuchumi kwa maslahi ya watawala na tabaka ambalo linazimiliki nyenzo za uzalishaji mali (uk 39).
    • Bwana Kangata na jamii yake walilowea kwa shamaba la mwajiri wao ambaye alikuwa akiishi jijini (uk 64).
    • Kimondo alimweleza Lunga kuwa kuishi kwao wanyonge kuliamuliwa na matajiri (uk 69).
    • Waafrika wafanyakazi maskini walinyimwa matibabu kwa kukosa Medical Scheme kama alivyoeleza daktari mwafrika (uk 70).
    • Baada ya wakimbizi kuishi katika Msitu wa Mamba kwa kipindi fulani, jamii ilianza kutwaa uchangamano wa mtu kutambua kuwa yeye alitokana na ukoo mtukufu na jirani yake alikopolewa na ukoo wa mlalaheri (uk 75).
    • Katika wimbo wake, Shamsi anaeleza kuhusu matajiri wanaomchungulia na kumcheka wakiwa kwenye roshani zao wakipunga pepo baada ya kujaza matumbo yao (uk 130).
    • Ridhaa alihamia mtaa wa Afueni. Mtaa wa watu wenye kima cha juu kiuchumi. Daraja kubwa limeutenga mtaa huu na mtaa wa Kazikeni, mtaa wa watu wenye maisha ya kubahatisha (uk 137- 138).(8×1= 8)

     Au
  2. Jadili nafasi ya sehemu zifuatazo katika riwaya ya Chozi la Hari:
   1. Hotuba (alama 10)
    • Hotuba ni maelezo maalumu yanayotolewa na mtu mmoja mbele ya watu. Pia huitwa hutuba. Mwandishi wa riwaya hii ametumia hutuba kwa ustadi mkuu kupitisha ujumbe mbalimbali. Hotuba hizi ni:
    • Hotuba ya Racheal Apondi kwa maafisa waliohudhuria warsha kuhusu jukumu la vikosi vya askari katika kudumisha usalama, amani na maridhiano nchini (uk 112- 113). Katika hotuba hii, Racheal Apondi anasisitiza kuwa:
     Suala la usalama haliwezi tena kupuuzwa. Usalama umekuwa mojawapo ya mahitaji ya kibinadamu.
     Anasema kuwa bila usalama, binadamu hawezi hata kushiriki katika shughuli za kuzalisha mali, hivyo hata mahitaji yake mengine ya kimsingi kama vile chakula, malazi na makazi hayawezi kukidhiwa.
     Kila binadamu ana jukumu la kudumisha amani na usalama.
     Wafanyakazi wa umma, hasa polisi na wanajeshi wana jukumu kubwa zaidi la kudumisha usalama na amani.
     Kila mmoja wetu anastahili kuhakikisha kuwa ameepuka vitendo vya kihalifu.Ni vyema mtu kuwaangaza wahalifu wakati wote.
     Vikosi vya polisi na wanajeshi vimefunzwa maarifa ya kukabiliana na kadhia za jinai na upelelezi. (4×1= 4)

    • Hotuba ya Lunga Kiriri- Kangata kwa walimu na wanafunzi gwarideni (uk 68-69). Hotuba hii ilisisitiza umuhimu wa kuhifadhi mazingira. Anasisitiza kuwa:
     Suala la uhifadhi wa mazingira ni jukumu la kila mmoja wetu.
     Misitu ilikuwa imevamiwa na viongozi wenye mate ya fisi.
     Baadhi ya vinara wa taasisi mbalimbali za umma wamewaacha wanyama kama mayatima kwa kuwapoka makazi yao.
     Maelfu ya maekari ya misitu yamefyekwa na kujengwa viwanda.
     Badala ya mibambakofi na miti mingine inayosafisha hewa, michai imetwaa nafasi yake.
     Wanaohusika na matendo haya wanapoulizwa hudai kuwa michai si adui ya mazingira!
     Wengine wanasema kuwa misitu haina budi kukatwa ili kupanda mimea inayotoa chakula, kwani jamii lazima ijitosheleze kwa chakula.
     La kuhuzunisha ni kwamba hawa hawa wanaosema hivyo ndio wanaokita majengo ya kifahari katika sehemu ambazo zinastahili kutengewa upanzi wa chakula!
     Wengine wamediriki kunyakua hata madhabahu kwenye Mlima wa Nasibu ili kujenga hoteli kubwa za kitalii.
     Wazee wetu hata hawana mahali pa kuchomea kafara!
     Tunakata miti bila kupanda mingine.
     Hata mabustani ya maua tunashindwa kuyastawisha.
     Tukiendelea kuharibu mazingira sehemu yetu itazidi kuwa jangwa. (2×1= 2)
    • Hotuba ya Umu katika hoteli ya Majaliwasiku yake ya kuzaliwa.
     Umu anawashukuru Mwangeka na Apondi kwa kuwa wazazi wake wema.
     Anawashukuru kwa kumsomesha.
     Anawashukuru kwa kumsaidia Dick kujiendeleza kimasomo.
     Mwangeka na Apondi wanamshukuru Umu kwa kuwapa furaha.
     Apondi anamshukuru kwa kumlea mdogo wao kwa maadili bora. (2×1= 2)

    • Hotuba ya Dick katika hoteli ya Majaliwa siku ya kuzaliwa kwa Umu.
     Dick anamshukuru Umu kwa msaada wake na ahadi ya kumlea.
     Anamkumbusha siku walipokutana katika uwanja wa ndege na ilivyokuwa muhimu kwake.
     Anamshukuru Umu kwa kumwelekeza kwa wazazi wao wale.
     Anawashukuru Apondi, Mwangeka na wanawe kwa ushauri wanaompa. (2×1= 2)
     Mtahiniwa ataje hotuba kisha aeleze masuala muhimu yanayoibuliwa na kila moja.
   2. Uozo katika jamii (alama 10)
    • Uozo ni hali ya kuzorota na kutozingatiwa tena kwa maadili mema katika jamii. Ni hali ambapo milazote na desturi njema huvurugwa na wanajamii wanaofanya mambo yaliyo kinyume nahali halisi ya maisha. Mwandishi amejadili suala hili kwa undani kama ifuatavyo;
    • Jamii inaendeleza ubakaji. Genge la mabarobaro watano lilifululiza hadi walipokuwa maskini Lime na Mwanaheri na kuwabaka mbele ya baba yao (uk 25).
    • Kuna ulanguzi wa dawa za kulevya. Dick alipotoroshwa na Sauna alipelekwa kwa tajiri mmoja aliyemwingiza katika kusafirisha dawa za kulevya kutoka nchi moja hadi nyingine (uk 119- 120).
    • Wanajamii wanaendeleza uporaji na wizi wa mali. Vijana wanawavamia watu, kuwaua na kupora katika maduka ya kihindi, kiarabu na ya waafrika wenzao.
    • Jamii inaendeleza ufuska/ ukahaba. Sauna aliiba watoto na kuwapeleka kwa mama mmoja aliyewatumia kwa biashara ya nipe nikupe (uk 84).
    • Biashara haramu inaendelezwa. Bi. Kangara alifanya biashara ya kuwauza watoto na vijana- Safari yake ilipata mkondo mwingine baada ya polisi kupata fununu kuhusu njama ambazo yeye na Bi. Kangara walikuwa wakiendesha. Mabibi hawa walikuwa na mtandao ambao kazi yake ilikuwa kuwauza watoto na vijana (uk 84).
    • Kuna tatizo la mimba za mapema. Vijana wana mazoea ya kukumbatia mtafaruku wa kuhisia unaowapata na mara hujipata wameambulia ujauzito kama alivyofanya Zohali (uk 98).
    • Baadhi ya wanajamii wanaendeleza uavyaji mimba. Sauna alijaribu awezavyo kuavya mimba na mwishowe, baada ya kushindwa, anaamua kujiua.
    • Kukiuka maadili ya kikazi. Fumba (mwalimu) anakiuka maadili ya kazi na kujihusisha kwa mapenzi na mwanafunzi wake, Rehema, na hatimaye kumpachika ujauzito (uk 102).
    • Wazazi wanawabaka wana wao. Babake Sauna anafanya mapenzi na mwanawe kila apatapo nafasi, na mwishowe, Sauna anapata mimba.
    • Starehe na anasa kwa vijana. Vijana wa vyuo vikuu wameshindwa kutofautisha usiku na mchana. Tindi anasahau kumrejesha Lemi nyumbani kutokana na muziki (uk 121).
    • Wazazi wanakwepa malezi na kuwatupa wanao wakiwa wachanga. Neema anampeleka mtoto aliyemwokota kwa polisi (uk 162).
    • Vijana kuwaiga wazee. Mwangemi na Mwangeka walikuwa na tabia mbovu ya kumuiga babu yao (uk 186). (10×1= 10)
    • Mtahiniwa afafanue kwa mifano kutoka katika riwaya.

 3. SEHEMU YA C: HADITHI FUPI: TUMBO LISILOSHIBA NA HADITHI NYINGINE (AlifaChokocho na Dumu Kayanda- Wahariri)
  Jibu swali la Nne ama la Tano

  NDOTO YA MASHAKA
  1. “Sasa nimechoka mja. Nimechoka hata naradua kufa kuliko kuishi.”
   1. Eleza muktadha wa dondoo hili (alama 4)
    • Haya ni mawazo ya Mashaka. Yuko chumbani mwake. Anakumbuka hali yake ngumu ya maisha na mashaka tele. Anamkumbuke mkewe, Waridi, alivyomtoroka na wanawe. Anayaona maisha kutokuwa na thamani tena kiasi kwamba anaona kifo kingemfaa. (4×1= 4)
   2. Taja mbinu mbili za lugha katika dondoo hii (alama 4)
    • Takriri- nimechoka
    • Uzungumzi nafsi- sasa nimechoka… (2×2= 4)
   3. Mzungumzaji alikuwa na haki ya kuradua kufa. Thibitisha (alama 12)
    • Mashaka alikuwa na haki ya kuradua kufa kwani alikuwa amepitia matizo mengi:
    • Mamake mzazi, Ma Mtumwa, aliiaga dunia punde tu baada ya kumkopoa.
    • Baada ya kifo cha mamake, babake alishindwa kuvumilia naye akaaga dunia.
    • Mashaka alilelewa na Biti Kidebe asiyekuwa mamake mzazi.
    • Mamake mlezi, Biti Kidebe naye alihitaji kulelewa. Daima alilalamikia miguu yake.
    • Mashaka alilazimika kufanya vijikazi ili kumsaidia mamake mlezi kupata chohcote cha kutumia.
    • Mashaka na Biti Kidebe walipanda mabokoboko ambayo wengi waliamini si ndizi.
    • Biti Kideba alienda jongomeo pindi tu Mashaka alipomaliza chumba cha nane.
    • Mzee Rubeya na Shehe Mwinyimvua wanawafungisha Mashaka na Waridi Ndoa ya Mkeka bila kupenda kwao.
    • Mzee Rubeya wanawakimbia Mashaka na Waridi na kurudi kwao Yemeni ili Mashaka wasije kuwaaibisha.
    • Kazi ya Mashaka ilikuwa ya kijungu meko- ya kupigania tumbo.
    • Mashaka na Waridi waliishi sehemu kuchafu kule Tandale, Kwatumbo, eneo la Uswahilini.
    • Walikosa vyoo wakawa wanatumia karatasi kwa haja zao zote.
    • Mashaka na Waridi walipata watoto wengi, saba, ambao wanawashinda kuwakimu.
    • Mashaka alilazimika kuomba jikoni kwa jirana yake, Chakupewa, ili wanawe wa kiume wapate mahali pa kulala.
    • Chumba chao kiliingiza maji mvua iliponyesha.
    • Mashaka alifanya kazi ya usiku katika Shirika la Zuia Wizi Security (ZWS).
    • Waridi anamtoroka Mashaka maisha yanapokuwa magumu. (12×1= 12)
    • Kila hoja ifafanuliwe kikamilifu


     Au
  2. Ukirejelea hadithi zozote nne katika diwani ya Tumbo Lisiloshiba na Hadithi Nyingine, eleza jinsi maudhui ya Mapenzi na ndoa yanavyojitokeza (alama 20)
   1. Masharti ya Kisasa
    • Ndoa ya Dadi na Kidawa
    • Ndoa imedhibitiwa na masharti.
    • Kuna kugawana majukumu katika ndoa.
    • Ndoa zinazingatia mno kupanga uzazi.
    • Ndoa inaruhusu mwanamke kufanya kazi. Kidawa alikuwa Metroni.
    • Baadhi ya watu huingilia ndoa za wenzao ili kuvunja mapenzi ya wanandoa. (5×1= 5)
   2. Mapenzi ya Kifaaurongo
    • Ndoa iliyotarajiwa kati ya Dennis na Penina ilijaa unafiki. Penina anamfukuza Dannis kwa kukosa kazi.
    • Ndoa imetawaliwa na kuhimiliana.
    • Ndoa imejaa kukata tamaa. Penina anamfukuza Dennis baada ya kukosa kazi.
    • Ndoa imezingirwa na utabaka.
    • Mapenzi humea, hukua, huugua na kufa baadaye. (5×1= 5)
   3. Ndoto ya Mashaka
    • Ndoa ya Mashaka na Waridi
    • Ndoa ya Mtumwa na Mzee Rubeya
    • Ndoa ni ya kulazimishwa- Mashaka na Waridi
    • Utabaka umetawala ndoa- Waridi ni wa tabaka la juu
    • Ndoa inakumbwa a tatizo la malezi bora.
    • Kuna mateso na kutengana kwa wanandoa.
    • Ndoa zinakumbwa na matatizo mengi.
    • Ndoa za mapema ni chanzo cha aibu. (5×1= 5)
   4. Mtihani wa Maisha
    • Wazazi wa Samueli wanampenda sana mwanao. Wanampeleka shuleni ili apate elimu.
    • Samueli anampenda sana Nina.
    • Nina anamwamina sana Samweli na kuamini kuwa ni bingwa.
    • Mamake Samueli anampenda sana mwanawe. Anamtaka asijiue.
    • Ndoa humwitaji mwanamke kumheshimu mumewe.
    • Mtoto wa kike anachukuliwa kuwa si bora kama alivyo wa kiume. Babake Samueli aliamini kuwa motto wa kike akiolewa mambo yake huwa yameisha. (5×1= 5)
    • Mtahiniwa asirudie hoja moja katika hadithi zaidi ya moja. Kila hoja ifafanuliwe kikamilifu.

 4. SEHEMU YA D: USHAIRI
  Jibu swali la sita ama la saba
  1. MASWALI
   1. Lipe shairi hili anwani mwafaka. (Alama 1)
    • Naogopa (1×1= 1
   2. Eleza dhamira ya mtunzi wa shairi hili. (Alama 1)
    • Mtunzi alidhamiria kuonesha baadhi ya matatizo wanayoyapitia wanawake baada ya kufunga ndoa. (1×1= 1)
   3. Nani nafsi nenewa katika shairi hili? (Alama 1)
    • Nafsi nenewa ni mwanamume (mzee) anayetaka kufunga ndoa. (1×1= 1)
   4. Taja tamathali za lugha zilizotumika katika shairi hili (Alama 2)
    • Takriri- naogopa
    • Tashbi- wanauma ja panya
    • Msemo- wanauma ja panya wakipulizia
    • Taswira- naogopa nawe babu kusimama (2×1= 2)
   5. Fafanua uhuru wa ushairi alioutumia malenga (Alama 2)
    • Tabdila- mie- mimi
    • Inkisari- kwita- kuita
    • Kikale- mtima- moyo
    • Kufinyanga sarufi- matusi anipatie- anipatie matusi (2×1= 2)
   6. Weka shairi hili katika bahari mbalimbali (Alama 3)
    • Ukawafi- lina vipande vitatu katika kila mshororo
    • Kikwamba (zivindo)- neno ‘naogopa’ linarudiwa mwanzoni mwa kila mshororo.
    • Mtiririko- vina vya ndni na vya nje vinafanana kutoka ubeti wa kwanza hadi wa mwisho. (3×1= 3)
   7. Andika ubeti wa tatu kwa lugha nathari. (Alama 4)
    • Naogopa uchungu utakaoniuma ili nikuzalie mwana. Naogopa kupigwa kama ngoma ndiposa nitulie. Naogopa kuchunguzwa ndipo unipe pesa. Naogopa kuwa nitaitwa mwizi wa sima ilhali nakuandalia. (4×1= 4)
   8. Kwa nini nafsi neni anasita kuchukua hatua? (alama 4)
    • Hataki alie
    • Anaogopa wanaume kwani wanauma kama panya.
    • Anaogopa kuita mama ya mumewe mama naye amkaripie
    • Anaogopa dhuluma za wanaume
    • Anaogopa kushinda ameinama goti mume ampigie
    • Anaogopa mkemwenza amhujumu na kumtusi.
    • Anaogopa uchungu wa kujifungua.
    • Anaogopa kupigwa kama ngoma.
    • Anaogopa kusomwa kabla ya kupewa pesa.
    • Anaogopa kuitwa mwizi wa sima anayoandaa.
    • Anaogopa udaku wa dada za mume.
    • Anaogopa uhasama wa kupiganiwa
    • Anaogopa kushindania mali kortini
    • Anaogopa kufichua siri za kina bwana.
    • Anaogopa ndoto zake kuzizima na doa ajitie
    • Anaogopa kuizima taa yake (8× ½ = 4)
   9. Vifungu vifuatavyo vina maana gani katika shairi? (alama 2)
    • Taa yangu kuizima- kupoteza matarajio/ malengo yake
    • Dhuluma- mateso (2×1= 2)

     Au
  2. Soma shairi lifuatalo kasha ujibu maswali
   Maswali
   1. Hili ni shairi la aina gani ? Thibitisha (alama 2)
    • Shairi huru- Halijazingatia kanunu zote za utunzi wa mashairi wa kuzingatia arudhi (2×2= 2)
   2. Ni nani anayeimba shairi hili na analiimba kwa nani ? (alama 2)
    • Anayeimba ni mjomba
    • Anayeimbiwa ni mpwawe (2×1= 2)
   3. Toa ithibati kwenye shairi hili kuthibitisha kuwa msimulizi ana taasubi za kiume (alama 2)
    • Anaambiwa uoga ukimtikisa huenda ni wa akina mamaye
    • Alichinjiwa fahali ili awe mwanamume (2×1= 2)
   4. Taja kwa kutolea mifano mbinu zozote nne za uandishi katika shairi hili (alama 4
    • Chuku – wao hukatwa kuanzia macheo hadi machweo
    • Takriri – kikali
    • Isitiari – upweke ni uvundo
    • Tashhisi – uoga ukifikia (2×2= 4)
   5. Taja shughuli zozote mbili za kiuchumi za jamii inayorejelewa katika shairi hili (alama 2)
    • Wakulima – Atapewa shamba la mahindi
    • Wafugaji – Atapewa mbuzi (2×1= 1)
   6. Eleza kwa mifano, uhuru wa kishairi katika shairi hili (alama 4)
    • Tabdila – aamushwe – aamshwe
    • Inkisari – Mme – mwanamume
    • Kuboronga sarufi – Fahali tulichinja- tulichinja fahali (2×2= 4)
   7. Msamiati ufuatao umetumika kwa maana gani katika shairi hili ?(alama 4)
    • Mbari- ukoo
    • Msununu- anayenuna
    • Ngariba- mtahirishaji
    • Uvundo- harufu mbaya (4×1= 4)

 5. SEHEMU YA E: FASIHI SIMULIZI
  1. Soma utungo ufatao kasha ujibu maswali
   Maswali
   1. Tambua kipera hiki cha fasihi simulizi (alama 2)
    • Maapizo- miungu na wakuone/ laana wakumiminie (1×2= 2)
    • Kutaja al 1- kufafanua al
   2. Jinsia ya nafsi neni ni gani? (alama 2)
    • Mwanamke/ jinsia ya kike- ndimi nilompa uhai mwana unoringia (1×2= 2)
    • Kutaja al 1- kufafanua al 1
   3. Eleza sifa zozote sita za kipera hiki cha fasihi simulizi (alama 6)
    • Maapizo yalitolewa kwa watu ambao walienda kinyume na maagizo ya jamii zao; wabakaji, waliowatusi wazazi wazee na wengineo.
    • Katika baadhi ya jamii za Kiafrika, maapizo yalitolewa kabla ya ulaji wa kiapo.
    • Maapizo yanaweza kutolewa moja kwa moja na yule aliyeathirika.
    • Kidini, Mungu, miungu au mizimu huweza kutoa maapizo kuhusu mustakali wa mtu fulani.
    • Maapizo huaminiwa kuwa yataleta maangamizi kwa jamii, hivyo wanajamii hushauriwa kuyaepuka kwa
    • kutenda mema.Maapizo hutumia lugha fasaha. Lugha ya ulumbi.
    • Maapizo hutumia lugha kali inayonuiwa kujaza woga ili kuonya dhidi ya maovu. (6×1= 6)
   4. Fafanua umuhimu wa kipera ulichokitaja hapo juu katika jamii (alama 4)
    • Hutumiwa kama nyenzo ya kuwaonya wanajamii dhidi ya matendo hasi.
    • Hutambulisha jamii. Kila jamii ina namna yake ya kuapiza.
    • Hukuza umoja katika jamii. Kuwapo kwa kaida na miiko sawa huwafanya watu kujihisi kuwa kitu kimoja.
    • Huadilisha. Wanajamii hujifunza kutenda mema ili kuepuka laana. (4×1= 4)Mtahiniwa afafanue hoja
    • zake ili zilingane na kipera cha maapizo.
   5. Fafanua njia sita jinsi jamii ya kisasa inavyojaribu kuendeleza fasihi simulizi (alama 6)
    • Wanafunzi hukariri, hughani na kuimba mashairi katika tamasha za muziki.
    • Mawaidha na vipera vingine vya fasihi simulizi hupitishwa katika sherehe za harusi, jando, mazishi na matambiko.
    • Utegaji na uteguaji vitendawili kupitia redio na runinga.
    • Michezo ya kuigiza katika runinga na redio.
    • Sarakasi zinazofanywa na wasanii huhifadhi kipera cha vichekesho.
    • Watafiti wanatafiti na kuhifadhi kwa kurekodi au kuandika vipera vya fasihi simulizi.
    • Utambaji wa hadithi bado hufanyika katika baadhi ya jamii, hasa katika sehemu za mashambani. (6×1= 6)

Download Kiswahili Paper 3 Questions and Answers - Form 4 Mid Term 2 Exams 2021.


Tap Here to Download for 50/-
Why download?

 • ✔ To read offline at any time.
 • ✔ To Print at your convenience
 • ✔ Share Easily with Friends / Students


Join our whatsapp group for latest updates
Get on WhatsApp Download as PDF
.
Subscribe now

access all the content at an affordable rate
or
Buy any individual paper or notes as a pdf via MPESA
and get it sent to you via WhatsApp

 

What does our community say about us?

Join our community on:

 • easyelimu app
 • Telegram
 • facebook page
 • twitter page
 • Pinterest