Kiswahili Paper 1 Questions and Answers - Form 4 Opener Term 1 Exams 2022

Share via Whatsapp

KISWAHILI 
Karatasi Ya 1

Maagizo

  • Andika insha MBILI. Insha ya KWANZA ni ya LAZIMA.
  • Chagua insha moja nyingine kutoka tatu zilizobaki.
  • Kila Insha isipungue maneno 400.
  • Kila Insha ina alama 20.


Maswali

  1. Lazima :
    Wewe ni katibu wa jopo lililoteuliwa kuchunguza chanzo cha utovu wa usalama kijijini Sokoto. Andika ripoti maalum /rasmi kuhusu jambo hili.
  2. Magonjwa mengi yanasababishwa na mitindo ya kisasa ya maisha. Jadili.
  3. Tunga kisa kitakachodhihirisha maana ya methali: Mchagua nazi hupata koroma.
  4. Andika insha itakayoanza kwa maneno haya:
    Milipuko mikubwa ilisikika pu! Pu! Puu! Kisha niliwaona watu wakikimbia kuelekea pande zote.


Mwongozo wa Kusahihisha

  1. Atambue kuwa ni swali la ripoti rasmi. Lazima insha hii iwe na anwani iliyo wazi, yaani iwe na neon ripoti, ya nani, kuhusu nini na wapi ?
    Sharti sura ya ripoti maalum au rasmi izingatiwe:Kichwa, utangulizi, taratibu/yaliyoshughulikiwa, mwili/matokeo ya uchunguzi,hitimisho,mapendekezo na sahihi.
    Baadhi ya hoja:
    • Insha iwe na maudhui yasiyopungua matano. Baadhi ya hoja ni kama vile:
      1. Ulevi
      2. Ukosefu wa kazi
      3. Wanyama wa pori kama vile ndovu
      4. Watoto kutopelekwa shule
      5. Utepetevu wa vyombo vyombo vya usalama
      6. Adhabu nyepesi zinazotolewa na mahakama
      7. Wazazi kutotekeleza wajibu wao kwa watoto
      8. Tamaduni zilizopitwa na wakati kama tohara, wizi wa mifugo n.k
    • Sharti mtahiniwa atoe mapendekezo ya kutatua tatitzo hili k.v
      1. Kupiga marufuku utengenazaji na unywaji wa pombe haramu
      2. Kuanza miradi ya kuajiri vijana
      3. Watoto wote kupelekwa shule
      4. Vyombo vya usalama kuwa macho na kupigana na uhalifu
      5. Adhabu kali kutolewa kwa wahalifu
      6. Wazazi kutekeleza wajibu wao wa kutunza watoto
      7. Kukabiliana vikali na makundi haramu
      8. Kutupilia mbali tamaduni zilizopitwa na wakati
    • Asiyezingatia sura ya ripoti aadhibiwe kwa kuondolewa 4s
    • Makosa ya sarufi na hijai yaadhibiwe yanapotokea
  2. Mtahiniwa aandike insha ya hoja
    1. Sharti ataje hoja, kuifafanua na kuitolea mifano
    2. Lazima aunge mkono hoja aliyopewa
    3. Pia aonyeshe upande wa pili wa hoja aliyopewa.
    4. Aeleze mitindo ya maisha ya kisasa.
    5. Hoja zake ziwe tano au zaidi
      • Hoja za kuunga mkono:
        1. Baadhi ya vyakula hasa vyenye mafuta, madini,sukari na chumvi husababisha magonjwa kama vile msukumo wa damu na kisukari
        2. Kukosa mazoezi ya mwili hasa kwa sababu ya matumizi ya magari ya usafiri na ya kibinafsi na watu hawatembei kwa miguu.
        3. Matumizi ya pombe huleta madhara mengi kwa mwili yanayosababisha magonjwa ya akili.
        4. Mienendo mibaya hasa kushiriki mapenzi ovyo ovyo husababisha magonjwa ya ukimwi, kisonono na magonjwa mengine ya zinaa.
        5. Uchafuzi wa mazingira husababisha magonjwa kama vile ya pumu,malaria ,kipindupindu n.k
      • Hoja za kupinga:
        1. Atetee kwamba magonjwa hayasababishwi tu na mitindo ya maisha ya kisasa.
        2. Baadhi ya magonjwa hurithishwa katika familia.
        3. Kuna magonjwa yanayoletwa na wadudu kama vile mbu, konokono n.k
        4. Magonjwa kama vile mafua husababishwa na hali ya anga na si hali ya maisha.
        5. Hali za kimaumbile kama vile mafuriko husababisha magonjwa kama vile kipindupindu.
  3. Sharti aelewa kuwa ni methali.
    • Atunge kisa ambacho kinaoana vizuri na maana ya matumizi ya methali hii.
    • Kisa chake kiwe cha kuvutia.
    • Sharti aonyeshe pande mbili za methali.Aonyeshe mhusika anayechagua kitu au jambo zuri lakini analikosa na kupata lingine la kiwango cha chini.
    • Anatakiwa kuonyesha kuwa tusiwe watu wa kuchagua vitu bali tufanye bidii kupata tunachokihitaji.
    • Makosa ya hijai na sarufi yaadhibiwe yanapotokea
  4. Ni sharti mtahiniwa aanze kwa maneno aliyopewa.
    • Anatakiwa kuanza kwa maneno yale bila ya kubadilisha wala kuyapunguza.
    • Kisa chake kiwa cha kuvutia na aonyeshe ni matukio yapi yaliyosababisha milipuko ile, kulikuwa na majeruhi na watu walitoroka kwenda wapi? Ni nini kilichotokea baada ya hapo?
    • Asipoanza kwa maneno aliyopewa atuzwe alama ya bakshishi

BK01
USAHIHISHAJI KWA JUMLA

Sharti mtahiniwa ajibu maswali mawili pekee.
Kazi ya mtahiniwa iwe nadhifu na ipangwe vizuri kiaya.
Makosa ya hijai na sarufi yaadhibiwe yanapotokea.
Baada ya kusahihisha kazi ya mtahiniwa, awekwe kwenye viwango ya A-D vilivyowekwa na baraza la kitaifa la mitihani K.N.E.C
Mtahini atakayepotoka, atakayejitungia swali au atakayetumia lugha isiyo Kiswahili atuzwe alama ya BK01.
Urefu wa insha sharti uzingatiwe (maneno 400) 14Urefu ukadiriwe hivi:

Tanbihi:

  1. Hizi ndizo alama za juu iwapo mtahiniwa ameandika kiwango hicho cha maneno . Kisha aadhibiwe makosa mengine
  2. Mtindo wa zamani wa kuondoa alama 2U ulitupiliwa mbali.

Alama zifuatazo zitumiwe katika usahihishaji.

√ Msamiati unaofaa
× Msamiati usiofaa
−Kosa la hijai
═Kosa la sarufi
^Alama ya achwa – neno linapoachwa katika sentensi

MWONGOZO WA VIWANGO.
Karatasi hii imedhamiria kutathmini uwezo wa mtihani wa kuwasiliana na msomaji na kuwasilisha ujumbe kimaandishi, akizingatia mada aliyopewa. Mawasiliano haya yatategemea ukwasi wa lugha ya mtahiniwa. Kwa kutegemea maagizo ya swali lenyewe na umahiri wa lugha, ni lazima kutilia mkazo mtindo, mada na uwezo na mtahiniwa kufuata maagizo vilivyo.

Mtahini lazima asome insha yote ili aweze kukadiria viwango mbalimbali vilivyopendekezwa, yaani A, B, C ama D kutegemea mahali popote pale pafaapo kuikadiria insha ya mtahiniwa.

VIWANGO MBALI MBALI

KIWANGO CHA D— MAKI 01 - 05.

  1. Insha ya aina hii haieleweki kwa vyovyote, ama uwezo wa mtahiniwa wa kutumia lugha ni hafifu sana hivi kwamba mtahini lazima afikirie kile anachojaribu kuandika.
  2. Mtahiniwa hana uwezo wa kutumia maneno ya Kiswahili kwa njia inayofaa.
  3. Lugha imevurugika,uakifishaji usiofaa na insha ina makosa ya kila aina ya kisarufi, kimaendelezo, kimtindo n.k.
  4. Kujitungia swali na kulijibu.
  5. Insha ya urefu \.warobo ikadiriwe hapa.

NGAZI MBALIMBALI ZA KIWANGO CHA D
D - (Kiwango cha chini) Maki 01 - 02.

  1. Insha haina mpangilio maalum na haieleweki kwa vyovyote vile.
  2. Kujitungia swali tofauti na kulijibu.
  3. Kuandika kwa lugha isiyo Kiswahili au kuchanganya ndimi.
  4. Kunakili swali au maswali na kuyakariri.
  5. Kunakili swali au kichwa tu.

D (Wastani)
Maki 3

  1. Mtiririko wa mawazo haupo.
  2. Mtahiniwaamepotoka kimaudhui.
  3. Matumizi ya lugha ni hafifu mno.
  4. Kuna makosa mengi ya kila aina.

D+ (D YA JUU) MAKI 04 - 05

  1. Insha huwa na makosa mengi ya kila aina, lakini unaweza kutambua kile ambacho mtahiniwa anajaribu kuwasilisha.
  2. Hoja hazikuelezwa kikamilifu / mada haikukuzwa vilivyo.
  3. Mtahiniwa hana uhakika wa matumizi ya lugha.
  4. Mtahiniwa hujirudiarudia.
  5. Insha itakayozingatia sura lakini ikose maudhui ikadiriwe hapa.

KIWANGO CHA C KWA JUMLA MAKI 06 -10.

  1. Mtahiniwaanajaribu kushughulikia mada japo hakuikuza na kuiendeleza vilivyo.
  2. Mtahiniwaanawasilisha ujumbe kwa njia isiyovutia / hana ubunifu wa kutosha.
  3. Mtahiniwa anaakifisha sentensi vibaya.
  4. Mtiririko wa mawazo unaanza kujitokeza japo kwa njia hafifu.
  5. Insha ina makosa mengi ya sarufi. ya msamiati na ya tahajia (hijai)
  6. Insha yenye urefu wa nusu ikadiriwe hapa.

NGAZI MBALIMBALI ZA KIWANGO CHA C
C - (C YA CHINI MAKI 06 - 07

  1. Mtahiniwa ana shinda ya kuwasilisha na kutiririsha mawazo yake.
  2. Mtahiniwa hana msamiati wa kutosha wala miundo ya sentensi ifaayo.
  3. Mtahiniwa anafanya makosa mengi ya sarufi, ya hijai na ya msamiati na insha haieleweki Kwa urahisi.

C WASTANI MAKI 08

  1. Mtahiniwa anawasilisha ujumbe lakini kwa njia hafifu.
  2. Dhana tofauti tofauti hazijitokezi wazi.
  3. Mtahiniwa hana ubunifu wa kutosha.
  4. Mtiririko wa mawazo ni hafifu na hana ufundi wa lugha unaofaa.
  5. Amejaribu kuishughulikia mada aliyopewa.
  6. Ana shida ya uakifishaji.
  7. Anafanya makosa mengi ya sarufi, ya hijai na ya msamiati lakini bado insha inaeleweka.

C+ (C YA JUU) MAKI 09 -10

  1. Mtahiniwa anawasilisha ujumbe vizuri akizingatia mada lakini kwa njia isiyokuwa na mvuto.
  2. Dhana tofauti tofauti zimejitokeza japo kwa njia hafifu.
  3. Kuna mtiririko wa mawazo japo hana ufundi wa lugha unaofaa.
  4. Misemo na methali zimetumika kwa njia hafifu.
  5. Ana shinda ya uakifishaji.
  6. Kuna makosa ya sarufi ya msamiati na ya hijai yanayoathiri mtiririko wa mawazo.

KIWANGO CHA B KWA JUMLA MAKI 11-15.

  1. Katika kiwango hiki, mtahiniwa anaonyesha hali ya kuimudu lugha.
  2. Mtahiniwa anatumia miundo tofautitofauti ya sentensi vizuri.
  3. Mtahiniwa ana uwezo wa kutumia lugha kwa ufasaha.
  4. Mada imekuzwa na kuendelezwa kikamilifu. Hoja zisipungue nne katika kiwango hiki.
  5. Insha ya urefu wa robo tatu ikadiriwe katika kiwango hiki.

NGAZI MBALIMBALI ZA KIWANGO CHA B.
B -(B YA CHINI) MAKI 11-12

  1. Mtahiniwa anawasilisha ujumbe vizuri kwa kueleza hoja tofautitofauti akizingatia mada.
  2. Mtahiniwa ana mtiririko mzuri wa mawazo.
  3. Mtahiniwa anatumia mifano michache ya msamiati unaovutia.
  4. Makosa yanadhihirika / kiasi.

B WASTANI MAKI 13

  1. Mtahiniwa anadhihirisha hali ya kuimudu lugha.
  2. Mawazo yake yanadhihirika akizingatia mada.
  3. Mtahiniwa anateua na kutumia mifano michache ya msamiati mwafaka.
  4. Sarufi yake ni nzuri.
  5. Makosa ni machache / kuna makosa machache.

B+ (B YA JUU) MAKI 14 -15

  1. Mawazo ya mtahiniwa yanadhihirika waziwazi.
  2. Mtahiniwa anawasilisha ujumbe kwa njia inayovutia na kwa urahisi akizingatia mada.
  3. Mtahiniwa ana mchanganyiko mzuri wa msamiati unaovutia.
  4. Sarufi yake ni nzuri. .
  5. Uakifishaji wake wa sentensi ni mzuri.
  6. Makosa ni machache ya hapa na pale.

KIWANGO CHA A KWA JUMLA MAKI 16 - 20.

  1. Mtahiniwa ana ubunifu wa mawazo yanayodhihirika na kutiririka akizingatia mada.
  2. Mtahiniwa anadhihirisha ujuzi wa lugha yenye mnato.
  3. Ana uwezo wa kutumia tamathali za usemi ili kutoa hisia zake kwa urahisi.
  4. Umbuji wake unadhihirisha ukomavu na ukakamavu wake kimawazo
  5. Insha ina urefu kamili.
  6. Maudhui hoja au mambo yanayozungumziwa,kuelezewa au kuhadithiwa kwa mujibu Mada iliyoteuliwa. }
  7. Maudhui ndio hasa uti wa mgongo wa insha yoyote ile.
  8. Ubunifu wa mtahiniwa hukisiwa kwa kutathmini uzito wa maudhui yake kulingana mada teule.

MSAMIATI.

  • Msamiati ni jumla ya maneno yatumiwayo katika lugha husika.
  • Mtahiniwa anatarajiwa kutumia msamiati unaooana na mada teule.
  • Kutegemea ukwasi wa lugha alionao, mtahiniwa anatarajiwa kuikuza mada kwa kuifinyanga lugha kiufundi.
  • Ni muhimu kuelewa kwamba kutokana na maendeleo na ukuaji wa teknolojia na mawasiliano maneno mapya yanaibuka kila uchao.

MTINDO.

  • Mtindo unahusu mambo yafuatayo:
  • Mpangilio wa kazi kiaya. .
  • Mtiririko na mshikamano wa mawazo kiaya na katika insha nzima.
  • Hati nzuri na inayosomeka kwa urahisi.
  • Matumizi ya tamathali za usemi, kwa mfano, methali, misemo, jazanda na kadhalika.
  • Kuandika herufi vizuri kwa mfano Jj, Pp, Uu, Ww na kadhalika.
  • Sura ya insha.
  • Unadhifu wa kazi ya mtahiniwa.

SARUFI.

  • Sarufi ndio msingi wa lugha. Ufanisi wa mawasiliano hutegemea uwezo wa mtahiniwa wa kutunga sentensi sahihi zenye uwiano wa kisarufi. Mtahini ataonyesha makosa yote ya sarufi yaliyo
  • katika insha anayosahihisha. Makosa ya sarufi huweza kutokea katika:
  • Matumizi ya alama za uakifishaji. .
  • Kutumia herufi kubwa au ndogo mahali pasipofaa.
  • Matumizi yasiyofaa ya ngeli na viambishi, viunganishi, nyakati, hali, vihusiano na kadhalika.
  • Mpangilio wa maneno katika sentensi.
  • Mnyambuliko wa vitenzi na majina.
  • Kuacha neno linalohitajika au kuongeza neno lisilohitajika katika sentensi.
  • Matumizi ya herufi kubwa: .
  • Mwanzo wa sentensi.
  • Majina ya pekee.
  • Majina ya mahali, maji, nchi, mataifa na kadhalika.
  • Siku zajuma, miezi n.k.
  • Mashirika, masomo, vitabu n.k.
  • Makabila, lugha n.k.
  • Jina la Mungu.
  • Majina ya kutambulisha hasa wanyama wa kufugwa, kwa mfano yale ya mbwa.- Foksi, Jak, Popi,
  • Simba, Tomi na mangineyo.
  • Majina halisi ya watu k.m Maria, Rutto.

MAKOSA YA HIJAI / TAHAJIA.
Haya ni makosa ya maendelezo. Mtahini anashauriwa asahihishe huku akiyaonyesha yanapotokea kwa mara ya kwanza tu. Makosa ya tahajia huweza kutokea katika;

  1. Kutenganisha neno kwa mfano ‘aliye kuwa’.
  2. Kuunganisha maneno kwa mfano ‘kwasababu’.
  3. Kukata silabi visivyo afikapo pambizoni kama vile ‘ngan-o’ badala ya nga-no.
  4. Kuandika herufi isiyofaa kwa mfano ‘ongesa’ badala ya ‘ongeza’.
  5. Kuacha herufi katika neno kwa mfano ‘aliekuja’ badala ya ‘aliyekuja’.
  6. Kuongeza herufi isiyohitajika kama vile ‘piya’ badala ya ‘pia’.
  7. Kuacha alama inayotarajiwa katika herufi kama vile j, i.
  8.  Kukosa kuandika kistari cha kuendelezea neno afikiapo pambizoni au kukiandika mahali pasipofaa.
  9. Kuacha ritifaa au kuiandika mahali pasipofaa, kwa mfano ngombe, ngom’be, ng’ombe, ngo’mbe n.k
  10. Kuandika tarakimu kwa mfano 27- 08- 2013.

ALAMA ZA KUSAHIHISHA.
== Hupigwa chini ya sehemu ambapo kosa la sarufi limetokea kwa mara ya kwanza tu.
___ Hupigwa chini ya sehemu au neno ambapo kosa la hijai limetokeza kwa mara ya kwanza tu.

  • Hutumiwa kuonyesha hoja inapokamilikia pambizoni kushoto.
  • Hutumiwa kuonyesha kuachwa kwa neno / maneno.
  • Hutumiwa kuonyesha msamiati bora. Alama hii hutiwa juu ya neno lenyewe.

X Hutumiwa kuonyesha msamiati usiofa. Alama hutiwa juu ya neno lenyewe.

Maelezo mafupi yanahitajika kuhusu tuzo lililotolewa. Kila ukurasa uwe na alama ya chini katikati ili kuthibitisha kuwa mtahini ameupitia ukurasa huo.
Maelezo yaonyeshe: Urefu wa insha k.v robo, nusu, robo tatu au kamili na udhaifu wa mwanafunzi.

UKADIRIAJI WA UREFU WA INSHA.
Maneno 9 katika kila msitari. Ukurasa mmoja na nusu
Maneno 8 kaitka kila msitari. Ukurasa mmoja na robo tatu.
Maneno 7 katika kila msitari. Kurasa mbili.
Maneno 6 katika kila msitari. Kurasa mbili na robo.
Maneno 5 katika kila msitari. Kurasa mbili na robo tatu.
Maneno 4 katika kila msitari. Kurasa tatu na robo tatu.
Maneno 3 katika kila msitari. Kurasa nne na nusu.

JUMLA YA MANENO.
Kufikia maneno 174 .lnsha robo.
Maneno 175 - 274 Insha nusu.
Maneno 275 - 374 Insha robo tatu.
Maneno 375 na kuendelea Insha kamili.

Join our whatsapp group for latest updates

Download Kiswahili Paper 1 Questions and Answers - Form 4 Opener Term 1 Exams 2022.


Tap Here to Download for 50/-




Why download?

  • ✔ To read offline at any time.
  • ✔ To Print at your convenience
  • ✔ Share Easily with Friends / Students


Get on WhatsApp Download as PDF
.
Subscribe now

access all the content at an affordable rate
or
Buy any individual paper or notes as a pdf via MPESA
and get it sent to you via WhatsApp

 

What does our community say about us?

Join our community on:

  • easyelimu app
  • Telegram
  • facebook page
  • twitter page
  • Pinterest