Kiswahili Paper 2 Questions and Answers - Form 4 End Term 2 Exams 2023

Share via Whatsapp
MAAGIZO
  • Jibu maswali yote
  1. UFAHAMU:( Alama 15)

Soma kifungu kifuatacho kisha ujibu maswali.

Meli alipokivuka kizingiti cha lango la shule ya kitaifa ya Tungambele alikuwa na azma ya kusoma kwa bidii ili kuinukia kuwa kijana wa kutegemewa na jamii yake. Alikuwa kalelewa katika familia yenye pato wastani. Akasoma kwa juhudi za wazazi wake hadi darasa la nane alipokwangura alama za kumwezesha kujiunga na shule hii ya kifahari. Meli alijua kwamba alikuwa mwanagenzi, si katika masomo ya shule ya upili tu, bali pia katika maisha ya jijini ambamo shule hii ilipatikana. Kwa kweli hii ndiyo ilikuwa mara yake ya kwanza kutia guu kwenye jiji hili ambalo habari zake akizisoma, ama katika magazeti machache yaliyowahi kufika kijijini, au kupitia somo la Elimujamii. Hata hivyo, Meli hakuwa mtu wa kuogopa au kunywea machoni mwa changamoto. Alijiambia kwamba kwa vyovyote vile atapambana na maisha haya mapya.

Saa mbili kamili asubuhi ilimpata Meli kapiga foleni katika afisi ya kuwasajili wanafunzi wageni. Wasiwasi wa aina fulani ulianza kumnyemelea alipotazama hapa na pale bila kuona dalili ya mja yeyote aliyemfahamu. Alijihisi kama yule kuku mgeni ambaye mwalimu wake alishinda kuwaambia kuwa hakosi kamba mguuni. Hata hivyo aliupiga moyo wake konde na kujiambia kuwa kuja kwake hapa kulitokana na juhudi zake mwenyewe na katu hatauruhusu ugeni wa mazingira kuifisha ari yake ya masomo.

Usajili ulikamilika, naye Meli na wenzake wakajitosa katika ushindani wa kimasomo jinsi waogeleaji wajitumbukizapo kidimbwini wakapiga mbizi, baadhi wakiambulia ushindi na wengine wakifedheheka kwa kushindwa. Meli na wenzake walibainikiwa kwamba wote walikuwa mabingwa kutoka majimbo na wilaya zao. Ilimbidi kila mmoja wao kujikakamua zaidi ili kuelea katika bahari hii ya ushindani. Muhula wa kwanza ulishuhudia kishindo cha Meli kubwagwa chini na majabali wenzake. Alijipata miongoni mwa wanafunzi kumi wa mwisho; au kama alivyozoea kuwatania wenzake katika shule ya msingi, “wanafunzi kumi bora kuanzia mwisho”! Hili lilimwatua moyo Meli na kumfanya kutahayari. Alifika kwao amejiinamia kama kondoo aliyeumia malishoni. Akawataka wazazi wake wambadilishie shule lakini wakakataa.

Muhula wa pili na wa tatu mambo yalikuwa yaleyale. Meli akahisi kama askarijeshi aliyeshindwa kabisa kutambua mbinu za kuwavizia maadui. Akaona kwamba njia ya pekee ni kujiunga na wenzake kama yeye katika vitendo vya utundu kama vile kuvuruga masomo kwa kupiga kelele darasani, kupiga soga bwenini na hata kuvuta sigara. Mwanzoni alichukia vitendo hivi lakini alimeza mrututu akisema kwamba ndiyo njia ya pekee ya kujipurukusha na aibu. Wazazi wa Meli hawakusita kutambua mabadiliko katika hulka ya mwanao. Wakajaribu kumshika sikio nyumbani lakini akawa hasikii la mwadhini wala la  mteka maji msikitini. Wakawahusisha wataalamu wa ushauri nasaha ambao waliwaambia kuwa Meli hakuwa na tatizo lolote la kuyadumu masomo. Kile alichokosa ni kujiamini tu.

Wazazi wa Meli waliona kuwa ni muhimu kuwahusisha walimu katika kutatua tatizo la mwanao. Mwanzo wa muhula wa pili uliwapata wazazi hawa afisini mwa naibu wa mwalimu mkuu. Mazungumzo kati ya wazazi, naibu wa mwalimu mkuu na mwalimu wa darasa la Meli yalidhihirisha kwamba walimu walikuwa wamemuasa Meli kuhusu kujiingiza katika makundi yasiyomfaidi lakini rai zao ziliingia katika masikio yaliyotiwa nta. Aliyopenda Zaidi Meli ni shughuli zilizomtoa nje ya shule kama vile tamasha za mziki, ukariri wa mashairi na drama. Mazungumzo yalibainisha kwamba Meli alihitaji ushauri na uelekezaji Zaidi kutoka kwa mtaalamu wa nasaha pale shuleni. 

Meli alianza vikao na mtaalamu huyu ambaye pia alimpendekezea Meli ushauri zaidi kutoka kwa washauri marika. Hili lilimchangamsha zaidi Meli kwani aliwaona hawa kama wenzake waliojua changamoto zake. Juhudi za mtaalamu wa nasaha na washauri marika zilifua dafu. Mwisho wa kidato cha pili ulishuhudia mabadiliko makuu katika hulka na utendaji kimasomo wa Meli. Aliukata kabisa uhusiano wake na marafiki waliompotosha na kuanza kuandamana na wanafunzi waliotia juhudi masomoni. Polepole alama zake ziliimarika. Matokeo ya mtihani wa kidato cha nne yalimweka kwenye safu ya wanafunzi bora zaidi nchini.           

  1. “Wanafunzi wawapo shuleni hukumbana na changamoto nyingi”. Thibitisha ukweli wa kauli hii kwa kurejelea hoja sita kutoka kwenye taarifa. .(alama 6)
  2. Eleza mchango wa washikadau mbalimbali katika kumsaidia Meli kupata ufanisi masomoni. (alama 4)
  3. Bainisha mbinu tatu za lugha ambazo msimulizi anatumia katika kuwasilisha ujumbe wake katika kifungu. (alama 3)
  4.  
    1. Andika kisawe cha ‘kijipurukusha’ kwa mujibu wa taarifa (alama 1)                                                                                   Andika
    2. Andika maana ya ‘kuwatania’ kulingana na taarifa. (alama 1)
  1. UFUPISHO  (ALAMA 15)

Soma kifungu kifuatacho kisha ujibu maswali.

Tangu kuripotiwa kwa maambukizi na vifo kutokana na Tandavu la Korona nchini Kenya, Wakenya wengi wamekuwa wakiishi kwa hofu. Vifo vinavyohusishwa na ugonjwa huu hatari vimekuwa vikiongezeka kila kukicha. Ugonjwa huu sugu unawafisha watu kwa muda mfupi baada ya kuambukizwa. Kutokuwepo kwa dawa za kutibu ugonjwa wenyewe kunaongeza wasiwasi miongoni mwa wanajamii. Nchi ya Kenya kama ilivyo mataifa mengine ulimwenguni imehimiza raia wake kupata chanjo dhidi ya tandavu hili. Hata hivyo, hatua ya serikali kutumia vitisho ili kuwashinikiza watumishi wa umma kupata chanjo ya korona haifai kwani huenda ikatatiza mpango wa kuchanja watu milioni kumi mwaka huu. Licha ya serikali kujaribu kuwalazimisha watumishi wa umma bado chanjo haijakubalika na wengi nchini. Kutokubaliwa kwa chanjo hii kumesababishwa na ukosefu wa elimu ya kutosha kuihusu. Watu wengi wanahofia kuwa huenda waliochanjwa wakapata madhara baadaye.

Mamilioni ya watu wameathiriwa kwa njia moja au nyingine na ugonjwa huu. Kenya imeshuhudia hoteli nyingi za kifahari kufungwa. Hii imetokana na usafiri wa ndege kusitishwa kote duniani. Kutokana na hali hiyo, hoteli zilizotegemea wateja watalii zilisimamisha shughuli zake kwa muda. Kwa mfano, ya Intercontinental ilifunga milango yake kabisa mwaka wa 2020. Jambo hili liliwafanya watu wengi kupoteza ajira.

Usafiri wa umma umekumbwa na changamoto si haba kutokana na tandavu la korona. Serikali ilipunguza wasafiri katika magari ya abiria kwa thuluthi moja. Wasafiri hao walilazimika kulipa nauli maradufu kwa safari ile ile. Watu wengi walilazimika kufutilia mbali mipango yao ya usafiri. Kafyu vile vile iliathiri usafiri huu wa umma. Magari mengi yalilazimika kusitisha safari njiani kwa kupatikana na kafyu. Wafanyabiashara katika sekta ya matatu wanahesabu hasara kubwa kwa kukosa abiria. Wengine wamelazimika kuuza magari yao kwa kutamaushwa na changamoto iliyowakumba ghafla.

Aidha, shule zililazimika kufungwa mnamo Machi 2020. Wanafunzi walikaa nyumbani hadi Januari 2021. Hii iliharibu kalenda ya masomo nchini. Serikali ilijaribu kuwasihi walimu kufunza mtandaoni lakini hii haikufaulu hata. Wanafunzi wa kike kadhaa waliishia kupata ujauzito hivyo basi kukatiza masomo yao. Ibada zote pia zilisitishwa. Nao waumini hawakusazwa. Baada ya serikali kufunga makanisa, misikiti na vyumba vingine vya ibada, waumini wengi walilazimika kufuatilia ibada zao katika runinga au mtandaoni. Waliokosa mitandao waliomba na jamaa zao na wengine kupuuza ibada hizo kwa muda.

Shida zilizindikana ugonjwa wenyewe ulipozidi kuenea. Hospitali za umma zililemewa na idadi ya wagonjwa waliokuwa wakienda kule kutafuta matibabu. Vitanda vilijaa na hata wengine wakalala chini katika wadi mbalimbali. Huduma za afya zikazidi kudidimia kutokana na ukosefu wa wahudumu wa afya na vifaa vya kutumiwa na wagonjwa. Vifo vingi vikaripotiwa katika hospitali hizi za umma. Kila sehemu nchini ikaathirika. Majonzi yakajaa kila mahali.

Licha ya haya mabaya yote yaliyokuja na ugonjwa huu wa corona, kuna wale waliochuma riziki kwa kuzuka kwa ugonjwa huu. Mambo mapya yalijitokeza katika ulimwengu wetu. Msamiati wa lugha ukaongezeka. Hii ilitokana na haja ya kuwepo kwa istilahi au misamiati ya kufafanua hali mpya iliyoibuliwa na tandavu hili. Vilevile Kutokana na watu kulazimika kufanya kazi nyumbani, ujuzi wa matumizi ya mtandao umeimarika. Kwa mfano, ufundishaji mtandaoni umefaidi vyuo vingi vinavyofundisha masomo ya mbali.

Wanabiashara wengine wakaanza kuuza barakoa. Barakoa ilikuwa kitu kigeni huku kwetu na duniani kwa jumla. Wengi walipata faida kubwa sana kwa kuwa soko la barakoa lilikuwa pana. Hata hivyo, barakoa zinazotumika na wananchi wengi hazijathibitishwa kuwa bora kuzuia korona. Hali hiyo inawafanya watumiaji wake kuwa na usalama wa bandia kwani wanaweza kuambukizwa ugonjwa wa korona kwa urahisi licha ya kuwa wamevalia barakoa hizo. 

Kadhalika, viyeyushi vikaanza kutumika kwa wingi humu nchini na duniani kote. Wachuuzi wengi waliingia biashara hii na kufaidika kiasi. Wengi hawakujua viyeyushi ni nini kabla ya wakati huo. Hivi sasa hata watoto wadogo wanajua viyeyushi na kutumia kwa njia mwafaka.

Kundi lingine lililonawiri kwa korona ni hospitali za kibinafsi. Wengi wa matajiri walioambukizwa ugonjwa huu walijipeleka hospitali hizi kwa matibabu. Wenye hospitali hizo nao wakapandisha bei ya matibabu kwao. Ikawa ni biashara inayonoga kabisa. Hawakujali kuhusu wale wasio na pesa. 

Korona imefanikisha juhudi za maafisa wa afya kuhimiza usafi kila mara. Hii ni kwa sababu watu wanalazimika kunawa mikono yao kila mara. Usafi huu wa mikono unapunguza visa vya magonjwa kama vile kipindupindu katika jamii. Aidha, gharama za sherehe zimepungua mno kutokana na sheria za kudhibiti idadi ya watu wanaohudhuria sherehe za mazishi au matanga. Hali hii ni nafuu kwa wale wachochole ambao wakati mwingine hulazimika kuuza kidogo walicho nacho ili kugharamia sherehe za matanga au arusi. 

UFUPISHO.

  1. Kwa kuzingatia aya tano za kwanza, eleza shida zilizoletwa na korona. (Maneno 100) (alama 9)
    Matayarisho.
    Nakala safi.
  2. Fupisha aya nne za mwisho kwa maneno 60. (alama 6)
    Matayarisho.
    Nakala safi.
  1. MATUMIZI YA LUGHA.
  1. Taja sauti zenye sifa zifuatazo. (alama 2)
    1. King’ong’o cha mdomo:-----------------------------------------------------------------------------------
    2. Irabu ya mbele kati:---------------------------------------------------------------------------------------
    3. Kipasuo ghuna cha kaakaa laini:------------------------------------------------------------------------
    4. Kikwamizo sighuna cha menoni:------------------------------------------------------------------------
  2. Dhihirisha miundo ya silabi katika maneno yafuatayo. (alama 2)
    1. itwa:------------------------------------------------------------------------------------------------------------
    2. Mchwa:------------------------------------------------------------------------------------------------------
  3. Tunga sentensi mbili ili kuonyesha matumizi ya kiakifishi  (alama 2)
    Vifungo
  4. Tunga  sentensi ukitumia: (alama 2)
    1. Kihusishi cha ulinganisho
    2. Kihisishi cha kinyume cha matarajio
  5. Ainisha matumizi ya kiambishi “ji” katika sentensi (alama 3)
    Jibwa hilo liliweza kujinusuru kutokana na hasira za mkimbiaji.
  6. Andika sentensi ifuatayo katika wakati ujao hali timilifu.                          (alama 2
    Waziri anasoma hotuba yake.
  7. Tunga sentensi yenye kishazi kirejeshi ambacho ni kivumishi.              (alama 2)
  8. Andika sentensi ifuatayo katika hali ya ukubwa.
    Nyundo hizo zimetupwa mbali na jumba lile.                                                (alama 2)
  9. Tunga sentensi yenye muundo ufuatao:                                                     (alama2)
    Nomino ya wingi , kivumishi kiashiria, kitenzi kishirikishi, kielezi cha kiasi jumla’
  10. Changanua kwa vishale: Wale wageni wetu watakuwa wamewasili leo jioni. Al4
  11. Bainisha yambwa na chagizo katika sentensi inayofuata.                                            (Al 2)
    Vibarua wamefanya hiyo kazi haraka iwezekanavyo.
  12. Badilisha sentensi katika kauli iliyomo kwenye mabano.
    1. Marie alipewa zawadi yake. (tendeka)                                                              (alama 2
    2. Tunga sentensi ukitumia kitenzi kishirikishi kipungufu katika ngeli ya KI-VI.  (alama 2)
  13. Tofautisha matumizi ya ‘Ngali’ katika tungo hizi. (alama 2)   
    Mama angali mlimani
    Otiende angalisoma kwa bidi angaliishi maisha mema.
  14. Andika sentensi katika wakati usiodhihirika ukitumia nomino moja ya jamii.                  (alama 2)
  15. Ainisha mofimu katika neno lifuatalo
    Hakumjia
  16. Tunga sentensi moja kutofautisha maana ya baba na papa                                  (alama 2)
  17. Methali: Haraka haraka haina baraka huambiwa mtu aliye na kasi isiyofaa katika kutenda mambo.Mtu anayepuuza shida za wenzake huambiwa aje?  Al2
  18. Biwi ni kwa taka ……………………ni kwa maji na kikuba ni kwa ………………. (alam2   
  1. ISIMU-JAMII                                                                                                               ISIMUJAMII
    … Bwana Spika, ninaomba kufahamishwa kwa nini Waziri wa Biashara ameshindwa kuchukua hatua kukomesha uuzaji wa vileo hatari kwa watoto wa shule.
    1. Fafanua sifa zozote tano za sajili inayorejelewa na maneno haya  al 5
    2. Eleza mambo yaliyochangia msambao wa Lugha ya Kiswahili kabla ya kuondoka kwa wakoloni barani.  Al5       

MARKING SCHEME

UFAHAMU

  1.  
    1. Meli kushindwa mtihanini na wanafunzi wenzake ingawa alikuwa na alama nyingi katika mtihani wa darasa la nane.
    2. Kutaniana. Meli alizoea kutania wenzake katika shule ya msingi waliokuwa wa mwisho katika mtihani.
    3. Kuatuliwa moyo/ kuvunjika moyo kwa Meli baada ya kufeli katika mtihani.
    4. Kutahayari baada ya kushindwa na wenzake katika mtihani.
    5. Kupiga kelele darasani ili kuvuruga masomo ya wenzake darasani.
    6. Kupiga soga bwenini
    7. Kuvuta sigara kwa wanafunzi kama Meli shuleni.
    8. Meli kupuuza ushauri wa wazazi wake awapo nyumbani.
    9. Kutojiamini katika masomo.
    10. Meli kujiingiza katika makundi yasiyomfaidi.                               
    11. Meli kupenda shughuli zinazowatoa nje ya shule kama tamasha za muziki, ukariri mashairi na drama baada masomo.                   (zozote 6x1=6)
  2.  
    1. Wazazi wa Meli walijaribu kumshika sikio / kumshauri akiwa nyumbani kuhusu masomo. Walishirikisha mtaalamu wa ushauri nasaha.
    2. Wataalamu wa ushauri nasaha walisema Meli alikosa kujiamini masomoni.
    3. Walimu walimuasa Meli dhidi ya kujiunga na makundi yasiyomfaidi
      • Naibu wa mwalimu mkuu. -   
      • Mwalimu wa darasa la Meli
    4. Mtaalamu wa nasaha aliyemshauri Meli na kumpendekezea Meli ushauri wa washauri marika.
    5. Washauri marika – bidii zao zilimsaidia Meli kujiimarisha kimasomo alipojiepusha na marafiki waliompotosha.
      (Zozote 4x1)
  3.  
    1. Masimulizi kuhusu maisha ya Meli shuleni
    2. Misemo – kutia guu/ kupiga foleni/ piga moyo konde/ lilimwatua moyo n.k
    3. Methali – kuku mgeni hakosi kamba mguuni / hasikii la mwadhini wala la mteka maji msikitini.
    4. Urudiaji / takriri Meli na wenzake….
    5. Kinaya / kejeli “ wanafunzi kumi bora kuanzia mwisho”
    6. Tashbihi / tashbiha “… amejiinamia kama kondoo aliyeumia malishoni..”
    7. Taswira “Meli kufika nyumbani amejiinamia….”
    8. Sitiari ‘Majabali wa Meli – wale waliomshinda Meli mtihanini       (Zozote 3x1)
  4.  
    1. kujiepusha/ kujisahaulisha/ kujilinda/ kujiokoa (alama 1)
    2. kuwadhihaki/ kuwafanyia mzaha/ kuwakejeli/ kuwafyosa/ kuwafyoa.(alama 1)

UFUPISHO.

  1. Kwa kuzingatia aya tano za kwanza, eleza shida zilizoletwa na korona. (Maneno 100) (alama 9)
    1. Wakenya kuishi kwa hofu.
    2. Korona inafisha kwa haraka.
    3. Ugonjwa wa korona hauna tiba
    4. Serikali kutishia kusimamisha mishahara ya wafanyikazi wa umma
    5. Chanjo kukosa kuwafikia wote.
    6. Hoteli kadhaa kufungwa
    7. Kupunguka kwa idadi yaw au katika magari ya abiria hivyo basi faida kupunguka.
    8. Shule kufungwa kwa miezi tisa
    9. Maabadi kufungwa
    10. Vifaa vya hospitali kutotosha
    11. Vifo vingi kushuhudiwa
    12. Biashara nyingi kufungwa.
      Zozote 8 x1 = 8, Utiririko 1
  2. Fupisha aya nne za mwisho kwa maneno 60. (alama 6)
    1. kuimarika kwa ujuzi wa matumizi ya mtandao.
    2. Kuongezeka kwa msamiati wa lugha.
    3. Biashara ya barakoa kunawiri.
    4. Matumizi ya baadhi ya barakoa unawapa watu usalama bandia.
    5. Wachuuzi wa viyeyushi kufaidika
    6. Hospitali za kibinafsi kuchuma kwingi Zozote 4 x 1 = 4 Utiririko 1
    7. Kuimarika kwa usafi wa umma.
    8. Kupungua kwa gharama za sherehe.
      zozote 5 x 1 = 5
      utiririko = alama 1

MATUMIZI YA LUGHA.

  1.  
    1. m
    2. e
    3. g
    4. th                                  4 x ½  = (alama  2)
  2.  
    1. i – twa
      I  - KKI
    2. m – chwa
      K  - KKKI                   4 x ½ = alama 2
  3. Vifungo
    1. Kufungia nambari/tarakimu
    2. Kutoa maelezo ya ziada
    3. Kuonyesha kisawe cha neno
    4. Kufungia maelekezo katika tamthilia
      2x1 = alama 2
  4.  
    1. Kuliko, kama, sawa na, mithili ya
    2. Hoyee! Huraa!             (alama 2)
  5. Matumizi ya ji
    1. Ukubwa
    2. Kirejeshi cha mtenda
  6. Waziri atakuwa amesoma hotuba yake.
  7. Mtoto aliyekuwa analia amenyamaza
  8. Majundo hayo yametupwa mbali na jumba lile.                                (1x1)
  9. Maji hayo/haya/ yale ni/yalikuwa mengi/    (4x½=  2
  10. S------KN+KT
    KN----V+N+V’
    V---Wale.
    N---Wageni.
    V—Wetu.
    KT---t+T+RE.
    t ----__Atakuwa.        Al 4
    T—Wamewasili
    RE—leo jioni.  Al2
  11. Kazi --- kipozi.
    Haraka iwezekanavyo--- chagizo.         Al 2
  12.  
    1. Maria alipeka zawadi.
    2. Kiatu ki mezani. Al 2
  13. Mama angali mlimani.---- kitendo kinaendelea.
    Masharti kitendo cha kusoma kwa bidii kinategemea kile cha kuishi maisha mema. Hakuna uwezekano.
  14. Maji yapatikana kwa wingi.
  15. ha – kikanushi cha nafsi ya tatu umoja
    Ku – kikanushi cha wakati uliopita
    M – mtendewa
    j – mzizi
    i – kauli ya kutendea
    a – kiishio
    ½ x 6 = 3
  16. Baba alivamiwa na papa akiwa baharini.   (2x1
  17. Mzigo wa mwenzio ni kanda la usufi.     (1x1)
  18. Biwi ni kwa taka funda ni kwa maji na kikuba ni kwa maua.

ISIMUJAMII

… Bwana Spika, ninaomba kufahamishwa kwa nini Waziri wa Biashara ameshindwa kuchukua hatua kukomesha uuzaji wa vileo hatari kwa watoto wa shule.

  1. Fafanua sifa zozote tano za sajili inayorejelewa na maneno haya.                               (alama 5)
    1. Husheheni msamiati / istilahi maalum kwa mfano, hoja, Bw.Spika, kamati.
    2. Lugha ya Bunge huwa na fomula: Huanza, kuendelezwa na kuhitimishwa kwa namna fulani. (mtindo maalum wa uwasilishaji)
    3. Kuna kuchanganya msimbo / ndimi – Napenda kumpongeza Waziri wa Finance kwa kupiga marufuku matumizi ya plastic bags.
    4. Kuna kuhamisha msimbo / ndimi.
    5. Lugha sanifu – mahali rasmi / penye hadhi kubwa.
    6. Lugha ya adabu hutumiwa – hakuna matusi, lugha ya ukali.
    7. Sentensi huwa ndefu ndefu. (maelezo marefu) /ulumbi.
    8. Lugha hubeba mambo ya kisheria / kikatili.
    9. Urudiaji / takriri ya maneno.
    10. Kuna kukatizana usemi / kalmia – hoja ya nidhamu.
    11. Lugha yenye ishara nyingi kwa mfano, kuinama.
    12. Kuna kupokezana zamu za kuzungumza.
  2. Eleza mambo yaliyochangia msambao wa Lugha ya Kiswahili kabla ya kuondoka kwa wakoloni barani.      (alama 5)
    1. Dini (Kiislamu na Kikristo)
    2. Biashara (ya shanga, chumvi, nguo n.k)
    3. Elimu - Wamishenari, walitumia Kiswahili kufunza kazi za kiufundi.
    4. Utafiti – vitabu viliandikwa  / tafsiri zilifanywa.
    5. Utawala wa kikoloni – Wajerumani walisisitiza matumizi ya Kiswahili Tanzania.
    6. Vyombo vya habari – magazeti yalianzishwa kabla ya uhuru.
    7. Siasa / Vita vya pili vya Dunia – wanasiasa walitumia Kiswahili.
    8. Muziki – nyimbo zilitungwa kwa Kiswahili.
    9. Ujenzi wa reli ya Kenya – Uganda.
      (zozote 5×1=05)             
Join our whatsapp group for latest updates

Download Kiswahili Paper 2 Questions and Answers - Form 4 End Term 2 Exams 2023.


Tap Here to Download for 50/-




Why download?

  • ✔ To read offline at any time.
  • ✔ To Print at your convenience
  • ✔ Share Easily with Friends / Students


Get on WhatsApp Download as PDF
.
Subscribe now

access all the content at an affordable rate
or
Buy any individual paper or notes as a pdf via MPESA
and get it sent to you via WhatsApp

 

What does our community say about us?

Join our community on:

  • easyelimu app
  • Telegram
  • facebook page
  • twitter page
  • Pinterest